Sunday, January 27, 2013

MSITU WA SOLONDO


 MSITU WA SOLONDO
'4'

Chapisho lililopita:
Golam amevutiwa na wasichana wale asiowajua kule msituni, waliokuwa wakimwita kwa mahaba. Golam akawafuata na kujiunga nao. Akapotea kimiujiza na badala ya sauti za mahaba sasa zikawa sauti za ajabu.
Nini kimempata Golam? Je, Golam atafanikiwa kurudi?
Endelea...

Amata alibaki kaweka mikono yake kichwani huku akitokwa na machozi, Saringo
Alishindwa kujizuia kulia kwa sauti na uchungu Hellen alimsaidia kumnyamazisha na kumpa moyo, Stephan alibakia akiangalia kwa mbali japo mkononi mwake alikuwa na bunduki yake kubwa lakini haikuweza kufanya chochote kwani pale walikutana na ulimwengu mwingine.
Upepo ulivuma taratibu usiku ule na moto uliendelea kuwaka taratibu, wakiwa wameuzunguka moto huo kila mmoja akiwa kimya akipanga na kupangua yaliyo kichwani mwake
“Msitu umemmeza...” Amata alisema kwa sauti ya upole
“One down, four to go!” Hellen aliongeza huku akirushia vijiti katika moto. Milio ya bundi na wanyama watawalao usiku vilisikika kutoka ndani kabisa ya msitu huo
“Masikini Golam!” alisikitika Saringo, Amata akamsogeza karibu na kumbana ubavuni kwake akimpa maneno ya faraja. Hellen aliinuwa mkono wake wa kushoto na kusoma saa yake iliyokuwa bado inajizungusha kuonesha wakati unavyokwenda, ilitimu saa kumi na nusu alfajiri, akavuta begi lake na kutoa kijiguduluia kidogo na kutengeneza kahawa ambayo wote walikunywa na kuchangamka upya. Alfajiri hiyo ilikuwa tulivu, kibaridi kilipuliza kwa upole, wote wanne walianza safari ya Solondo kwa siku ya pili,
 “Sasa tuwe makini zaidi maana tunazidi kuingia ndani ya msitu wa Solondo na tunakabiliwa na mauzauza mengi” Amata aliwasisitizia wenzake huku wakiendelea kukatisha pori lile nene, walikokuwa wakienda wote hawakujui isipokua tu kadiri ya maelekezo ya mchoro wa kale ambao mara nyingi Stephan na Saringo waliusoma uliwaelekeza upande Fulani na sasa uliwaekeza kuutafuta mbuyu mkubwa ambao upo huko ndani ya msitu na kwamba kutoka mbuyu huo ndio hasa atapata maelekezo sahihi ya wapi waelekee. Waliendelea mbele huku wakitumia panga kukata manyasi marefu yaliyofanya njia hiyo kuwa ngumu kupita. Amata aliyekuwa mbele alitumia ujuzi wake wote kukata manyasi hayo ambayo kana kwamba yliwasihi wasiendelee na safari yao ngumu. Wakiwa katia mwendo wa tabu sana dhidi ya nyasi ndefu na vichaka vya kutisha, miba mikali iliyowachoma na kuwakwangua kila upande wa miili yao lakini hawakukata tama hata kidogo, mara wakasikia mvumo kama wa wadudu wengi warukao, Amata alipoinua macho kutazama juu aliona mzinga mkubwa wa nyuki na wengi wakirandaranda huku na huko, Amata akawapa ishara wenzake kuonesha wawe watulivu dhidi ya nyuki hao wenye hasira. Helen alionekana kuchoka sana akiwa kamuegemea Stephan begani huku wakiendelea na safari yao
“Tupumzike kidogo” Stephan aliomba kwa kutumia Kiswahili chake cha kubabaisha, jua lilikuwa ni kali mno wakaketi chini ya mti mkubwa na kupumzika wakinywa maji na mikate waliyobeba.
“Amata, inaonekana safari za msituni unazijua sana eee!?” Saringo alimuuliza Amata
“Niliopokuwa na marehemu baba yangu tulikuwa tukienda kuwinda mara nyingi na yeye ndiye alinifundisha lugha na tabia ya msitu” Amata akajibu huku akiendelea kula mabungo aliyoyachuma porini.
“Lugha na tabia ya msitu! Ni vitu gani hivyo?” Saringo aliuliza kwa mshangao, akasogea karibu na Amata kana kwamba alitaka kujua vizuri juu y maneno hayo.
“Msitu huongea Saringo, na una tabia pia kama wewe ulivyo!” Amata alijibu “msitu una mambo mengi sana, hatari kubwa zipo, vyakula vingi vinapatikana na pia wanyama wa kuliwa na kula binadamu wapo” akamtazama Saringo aliyeonekena kuvutiwa na habari hiyo “pia msitu hukwambia juu ya hatari ijayo na ya namna gani, baba yangu alinifundisha haya yote kwa kuwa yeye kalelewa msituni robo tatu ya maisha yake” Amata alimalizia kusema.
“Ina maana wewe umeshawahi kuja huku Solondo?”Hellen alimtupia swali Amata
“Hapana, ni mara yangu ya kwanza kuja ndani kabisa ya msitu huu, na baba yangu aliniambia nisije kujaribu kuingia maana msitu huu unaaminiwa unakula watu, sikuwahi kuelewa kauli ile lakini sasa nimeijua maana yake!” Amata alimjibu Hellen
“Kwa vipi umeijua hiyo kauli?” Stephan alidakia
“Golam! Golam amemezwa na msitu” alijibu na kutikisa kichwa kuneshwa masikitiko yake, kisha akaendelea “tunakokwenda hatukujui lakini hatari kubwa iko mbele yetu, kwa kuwa tumeamua tuendelee, ila tusishangae tutakapopoteana huko mbele” Amata alimalizia kauli yake na kumtolea tabasamu Hellen akageuka upande wa pili kwa kuwa daima hakupenda kumwangalia Amata usoni maana tangu alipomuaona mara ya kwanza kule mtoni mara baada ya kutoroka gerezani alijikuta moyo wake ukimpenda ghafla kijana huyu, fukara asiye na dira ya maisha lakini mzuri wa uso na siha ya kiuanaume zaidi ya hapo kwa ujasiri mkubwa alionao wa kupambana na hatari na kujitolea mhanga, hilo ni swala ambalo Hellen lilizidi kuongeza mapenzi kwa Amata tatizo tu ni kuwa pale alikuwa na mchumba wake Stephan hivyo hakuthubutu kabisa kuonesha hali hiyo, na mara nyingi Saringo alipokuwa jirani na Amata, Hellen alisumbuka sana moyoni.
Stephan aliinuka pale alipoketi na kuchukua kimkoba chake kidogo ambacho ndani yake kulikuwa na kibuyu kidogo akaenda karibu na kijito kidogo umbali wa kutupa jiwe, kijito kile kilichosongwa na mitete mingi kilikuwa na maji machache yakitembea kwa taratibu sana. Alipofika pale alichota maji na kujaza kibuyu chake, kisha akaanza kutoa nguo zake ili apate kujimwagia maji. Amata akiwa kwenye maongezi na Saringo na hellen mara Amata akanyamaza ghafla na kutaza kwenye mitete ile akamuonesha ishara saringo ya kumuomba uta wake, amata aliupokea na kujiweka vyema
“Nini Amata?” Hellen alimuuliza
“Chatu! Nyoka mkubwa anayeweza kumeza mtu” Amata alijibu. Hellen akajificha nyuma ya Amata, Saringo alikuwa akiangalia kwa makini lakini hakuweza kuona cha kufanya alisubiri kuona nini Amata anataka kufanya, kwa upole Amata aliweka mshale  sawia katika uta wake na kuvuta kwa nguvu zake zote, mikono yake iliyojaa misuli ya nguvu ilituna na kuonesha kiasi gani nguvu alizotumia kuvuta uta huo, huku akiongea lugha isiyoeleweka akiwa ameuma meno bado hakuachia pigo lake, kilichoonekana ni jinsi tu alivyoutembeza uta huo taratibu sana kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Kutoka ndani ya mitete ile nyoka mkubwa alifyatuka kwa spidi ya ajabu kuelekea alipo mtoni alipo Stephan, Amata aliachia uta wake na mchale uliondoka kwa spidi kali kukikabili kichwa cha nyoka yule, hamad!!
“Stephannnnnnn!!!!!” Hellen alipiga kelele ya nguvu na Stephan alipogeuka alishuhudia joka kubwa refu lililofungua domo lake likimuelekea, mara alishuhudi kitu kikipita kwa kasi kati yake na joka lile, ulikuwa mshale wa Amata aliopigwa kwa ustadi lakini kutokana na ukelele wa Hellen Joka lile liligeukia upande ulikotoka ukelele hivyo kufanya shabaha ya Amata kuwa ya bure. Joka lile lilijivuta na kuburizika chini likijikunjakunja kuelekea walipo akina Amata, Amata alijinyanyua na kujirusha upande wa pili akimvuta Saringo wakati huo Helleni alijiinua na kujikuta amechelewa, alipigwa ngwala maridadi sana na joka lile na kupaishwa juu, kabla hajafika chini joka lili lilimdaka kwa ustadi mkuwa na kujivirigwa mwilini mwake, likiwa linadondoka kwa kwa kasi, Amata alikuwa tayari kesha vuta uta wake na kuuwachia, shabaha ya ajabu! Mshale ule ulipenya sawasawa karibu kabisa na kichwa cha joka lile, kutokana na maumivu yale joka lile likamuachia Hellen na kudondoka chini Hellen nae akadondoka juu yake, Joka lile likajivuta tena kumkimbiza Amata, amata hakukimbia mbali bali aliuzunguka mti ule waliokuwa wamekaa huku akiweka vizuri mshale wake wa tatu alijikwaa na kuanguka vibaya, joka lile likamtia mkononi likamviriga vizuri, bahati nazuri mkono mmoja wa Amata ulikuwa nje ya mvirigo ule
“Amataaaaa....” Saringo aliita, na kumrushia kisu ambacho Amata alikidaka kwa ustadi mkubwa na bila kuchelewa alididimiza kisu kile kwenye sehemu ya mwili wa joka hilo, joka likajiinua juu likiwa bado halijamuachia Amata, Amata alisikia mlio mkali na alichokishuhudia ni damu iliyoruka kwa matone makubwa makubwa, joka lile halikuwa na kichwa tena, likaanguka kwa mshindo mkuu, ilikuwa ni risasi kutoka AK 47 iliyopigwa kwa ustadi wa hali ya juu na Stephan na kukitawanya kichwa cha joka lile na kukichanachana vibaya.
“Nice shot!!” Hellen alimsifu Stephan, wakakumbatiana na kubusiana kama ishara ya kupongezana. Saringo alimfuata Amata pale alipolala na kumsaidia kujitoa katika joka lile, haikuwa kazi rahisi kuukunjua mwili wa joka lile kubwa ambao kwa wakati huo ulikuwa bado umejiviriga katika mwili wa Amata. Helen na Stephan nao waliungana na Saringo katika kazi hiyo, mara wakafanikiwa na kumnasua Amata ambae uso wake ulikuwa umechafuka kwa damu ya joka lile, wakamlaza vizuri na kumuosha uso wake. Mikono laini ya Saringo ilipita usoni mwa Amata, Amata akajisttikisa kidogo na kuushika mkono wa Saringo
“Nini Amata?” saringo alimuuliza
“Mkono wako laini umenisisimua mwili...” Saringo akatabasamu aliposikia maneno hayo ya Amata
“Usianze Amata!” Saringo akasisitiza. Amata aliketi na kutazama vizuri huku na huku, akaokota uta na podo lake akaweka mgongoni... safari inaendelea!
Msitu ulizidi kuwa mnene mbele yao, lakini Stephan aliyekuwa na ramani ya wapi wanakokwenda alisisitiza kuelekea upande huo hata kama haukuwa na njia, walisonga mbele, panda milima, shuka, vuka mto pasua vichaka, mvua, jua vyote vilikuwa juu yao, chakula kikubwa kilikuwa ni matunda ya porini ambayo kwayo walijitosheleza na kujipatia vitamini za kutosha sio mpaka akuandikie daktari.
Jioni hiyo ya siku ya tatu mvua ilikuwa kubwa sana, radi zisizo na huruma zilipasua anga lote na kulifanyia michoro ya kutisha, hapakuwa na pa kujikinga wala kujificha, wote walitota miili hata nguo zao kugandamana na miili yao, walitetemeka kwa baridi kali ya msituni hata miguu ilishindwa kutoa ushirikiano na mwili mara nyingi ilikataa kusonga mbele, hakukua na lakufanya isipokuwa ni kujivuta hivyo hivyo, walitamani jua liwake haikuwa hivyo, walipanda wakoke moto lakini kila kitu kililowana, safari ilizidi kuwa ngumu kwani msitu wote ulifunikwa na ukungu mzito hata mwanga wa tochi haukufua dafu. Amata alisimama na kugeuka nyuma akawaonea huruma wenzake maana walikuwa wakitetemeka kupita maelezo. Saringo alimuendea Amata na kumkumbatia kwa nguvu huku akitetemeka, vivyo hivyo kwa Hellen na Stephan, walivuta hatua fupifupi japo kwa shida kujitafutia mahali pa kupumzika.
“Tukae humu mpenzi!” Amata alishtuka kidogo kusikia kauli hiyo toka kwa Saringo, alibaki kujiulizauliza maana hajawahi kuitwa mpenzi katika maisha yake. Amata alitazama na kuona pango pembezoni mwa mti kabla hajaamua cha kufanya Stephan na Hellen wakawa tayari wamejitoma ndani ya pango hilo lenye kiza,
“Amata twende!” Saringo alisema huku akimvuta mkono kuelekea pangoni, Amata alimvuta Saringo kwa nguvu na kumkumbatia kifuani mwake, akamkazia macho Saringo alimtazama Amata usoni kwa hasira lakini hakuwa na la kusema alizungusha mikono yake mgongoni kwa Amata na kuikutanisha kisha kuegemeza kichwa chake kifuani mwa Amata. Amata alitulia kimya kwa muda akiangalia lile pango waliloingia akina Stephan
“Saringo! Unafikiri hilo ni pango? Isije kuwa mtego tu” Amata alimuuliza Saringo
“Wenzetu wameingia wewe hutaki, Amata una nini twende!” Saringo alisisitiza
“Saringo! Mbona hatumsikii Stephan au Hellen hata kutuita!? Nina wasiwasi hili si pango la kawaida!” Amata aliposema maneno hayo Saringo akashtuka na kugundua kuwa ni kweli hawa viumbe wawili wangeshawaita lakini kimya yapata dakika kumi sasa, Saringo akamuachia Amata, akaokota kipande cha mti kilicho jirani hapo akakirushia ndani ya pango lile lakini hakusikia chochote hata mdondoko wa kipande cha mti, Saringo akajishika mdomo na kuanza kutoa machozi.

Nini kimewapata Stephan na Hellen?
Kwa nini Saringo alitoa machozi?

Usikose kusoma sehemu ya nne ya simulizi hii, mfuatilie Amata ga Imba ndani ya msitu wa Solondo...
0767 152 125

Tuesday, January 15, 2013

SIMULIZI MPYA... (trailler)


MWANAMKE MWENYE

JUBA JEUSI


Mtunzi: Amata Ga ImbaUsiku ule hali haikuwa nzuri sana kwa Bw. Punde Kishime, kwa kuwa tangu alipoingia ofisini kwake asubuhi na kukuta barua ya vitisho mezani, barua hiyo iliyoonekana kuletwa kwa mkono tu haikuwa na anuani yoyote ndani yake, alipomuuliza sekretari wake alijibiwa tu kuwa barua hiyo ilikuwa imepenyezwa chini ya mlango hivyo aliiokota na kuiweka mezani.
Akiwa amejilaza juu ya sofa kubwa sebuleni kwake jioni ile, Bw. Punde Kishime aligubikwa na mawazo mazito ambayo yalimtoa kijasho chembamba, maswali aliyojiuliza hayakuwa na majibu kabisa. Mke wake, Bi Sheiza alimkaribisha chakula cha jioni lakini hakuwa hata na hamu ya kula alihisi kuwa ameshiba japo alikuwa na masaa kama ishirini na nne bila kula, woga, hofu, maswali yasiyo na majibu vyote vilichukua nafasi kubwa kichwani mwake hata alipokunywa maji kiu haikumuisha kabisa. Alibaki sebuleni hapo akitazama TV hata wote walipoenda kulala.
Mara simu yake ya mezani iliita, mshtuko alioupata haukuwa wa kawaida alihisi mwili kufa ganzi na kuchoka ghafla, taratibu alijinyanyua kutoka katika sofa lile na kuelekea mezani kuichukua simu hiyo
“Hallo… halo… haloooo” aliita lakini simu ile haikujibiwa, akairudisha kwenye kikalio chake na kuegemea meza kwa mikono yake miwili, hakujua afanye nini, aondoke aiache familia? Haiwezekani! Asafirishe familia abaki peke yake? hamna uamuzi! Alitoka pale na kujitupa kochini akiwa hajui la kufanya. Akapata wazo bora aondoke na familia yake usiku ule, lakini aende wapi? Hajui!
Kabla hajakata shauri simu yake ikaita tena, mara hii ilipokelewa na sauti ya kike

“nahisi barua yangu umeipata! kaa tayari katika siku mbili hizi nitachukua mzigo wangu, rafiki yako kipenzi Bw. Chiwawa Chakwima nimeshamalizana naye, nenda kamtembelee atakupa salamu zangu!”simu ikakatika, kabla hata Bw Kishime hajaongea.
Bw. Kishime alibaki haelewi kinachoendelea, ‘nani huyu!?’ Alikosa jibu. Alitoka nje na kuingia kwenye gari yake aina ya Toyota Harrier, gari hii alipewa zawadi na rafiki yake mmoja kutoka Thailand alipokwenda kumtembelea, aliingia na kutia moto injini ikakubali, alipiga rivas taratibu na kukunja kona, kwa mwendo wa kasi aliondoka kuelekea Masaki, akiwa barabarani aliendesha gari kama kichaa, aliiacha barabara ya Old Bagamoyo na kuchukua ya Namanga kupitia ubalozi wa USA, akiwa haelewi chochote alikunja kona kali kushoto mpaka tairi zikapiga kelele, alipofika katika mataa ya st Peter akakuta lori la takataka limeziba njia, akapiga honi nyingi lakini lori lile halikutaka hata kusogea, akaamua kushuka kwenda kumfuata dereva, alipoiacha gari yake tu mbele yake walitokea watu wawili wakiwa na shortgun mkononi
“Ha ha ha ha Bw. Punde Kishime, mtu mkubwa! Kwa nini unadanganyika kitoto hivyo? Yaani wewe hujui kama rafiki yako Bw. Chiwawa yuko kikazi Saudia?” mmoja wao alisema. Hapo ndipo Bw. Punde akakumbuka kuwa ni kweli rafiki yake Bw. Chiwawa amesafiri, alijiona mpumbavu sana.
“Ninyi ni nani? Na mnataka nini?” aliwauliza,
“ha ha ha ha … utatujua taratibu lakini sisi ni wajumbe tu, mama ametutuma kwako…”  mwingine alijibu kwa sauti nzito huku wakipiga hatua za taratibu kumsogelea. Ghafla alihisi kitu kizito kimempiga kisogoni akaanguka katika lami.
Toyota Harrier... aina ya gari aliyotumia Bw Punde Kishime kutoka nyumbani kwake usiku ule.
Mfano wa gari ya Taka iliyotumika kumzuia Bw Punde Kishime


********************
Riyadh International Airport-Saudi arabia


Boeing 747-400 Jumbo Jet ya shirika la ndege la Uingereza ilikunja tairi zake kumi na nane na kuiacha ardhi ya Saudi arabia na kukata anga kuelekea Africa ya Mashariki, Bw. Chiwawa Chakwima alitulia vizuri kabisa katika kiti chake ndani ya VIP coach, mawazo, akili na moyo wake vilikuwa vikiwaza nyumbani Tanzania, pembeni yake aliketi msichana mrembo nywele zake ndefu zilifika mpaka katika viwiko vyake, macho yake ya mviringo yalimfanya Bw. Chiwawa ashindwe kuangalia mbele, alipogeuka tena kumwangalia msichana yule aliinua mguu na kukunja nne, Bw. Chiwawa akaingiza mkono katika katika mfuko wa shati akatoa business card  akampatia, mrembo yule akaipokea na kuihifadhi. Mara mhudumu wa ndege ile alipita na kusimama karibu na Bw Chiwawa, akaingiza mkono katika trey ya chini akatoa bahasha ndogo ya khaki akampatia, Bw. Chiwawa akaipokea akataka kuifungua roho yake ikasita kidogo, akaitia kwenye mfuko wake wa ndani wa koti, alipogeuka kumwangalia yule mhudumu hakumuona alikuwa keshaondoka, akaingiza mkono mfukoni aitoe lakini akasita kwa mara nyingine! Akatulia kwenye kiti chake akitafakari hili na lile, alipoangalia saa yake ilitimu saa tisa alfajiri alipata faraja kwani alijua masaa matatu yajayo atakuwa nyumbani Tanzania. Mara alipata shauku ya kuona ndani ya bahasha ile kulikuwa na nini, akaitoa na kuifungua huku moyo ukimwenda mbio, alipoichana alikuta kijikaratasi kidogo kilichosomeka ‘watch the movie’ akatoa tabasamu iliyofuatiwa na kicheko cha chini chini, akaona ni upuuzi tu labda haikuwa yake mtu mkubwa kama yeye ambaye ana matarajio makubwa katika nchi yake pia ni kigogo mwenye nafasi nyeti serikalini, akavuta glass yake iliyojaa ‘covousier’ pombe aliyoipenda sana. Mhudumu wa ndege alipita tena sasa alikuwa mwingine akasimama pembeni na kutoa CD 
  
"Courvoisier" pombe aliyotumia Bw Chiwawa

“Do you like to watch movie?” akauliza mhudumu huku akiiweka cd ile katika kijimeza kidogo mbele ya Bw. Chiwawa. Akaichukua akaigeuzageuza kisha akaitoa kashani na kutumbukiza kwenye kifaa maalumu cha kufanyia kazi hiyo, akanyanyua visikilizio akatia kichwani ili apate kusikia kilichomo, akaitazama yote kwa makini kisha akaitoa na kuirudisha kashani, akaiweka juu ya kijimeza kile akashusha pumzi kwa nguvu huku kijasho chembamba kikimtoka! Shughuli nzito. Akachukua ile cd na kuitia katika koti lake kisha akatulia kitini. Alipiga funda lingine la pombe yake huku akitafakari kwa makini. Akiwa katika wimbi la mawazo alishtuliwa na sauti nyororo ya mhudumu kutoka katika vipaaza sauti vya ndege hiyo kuwa wote wafunge mikanda, akajiweka tayari kwa shauku kufika nyumbani baada ya wiki mbili alizokuwa nazo huko katika nchi za kiarabu.
Boeing Jumbo Jet ilikanyaga ardhi ya Dar es salaam yapata saa kumi na mbili kamili asubuhi, abiria wote waliteremka na Bw. Chiwawa alipokelewa na kuongozwa moja kwa moja VIP. Akiwa ndani ya chumba cha VIP alikutana na watu mbalimbali waliokuwa wakimsubiri, baada ya hapo walikuwa tayari kuondoka uwanjani hapo, walitoka nje na kuingia kwenye gari maalumu kwani alitakiwa kufika Ikulu moja kwa moja kuonana na Rais kwanza. Msafara wa gari tatu uliondoka airport na kuchukua barabara ya Nyerere kueleke mjini kati.
Msafara uliendelea kwa mwendo wa wastani mbele ukitanguliwa na Hyundai ya polisi ikifuatiwa na BMW nyeusi ambayo ndio hasa ilimbeba Bw. Chiwawa na nyuma yao kulifuatiwa na Toyota Prado VX nayo nyeusi metallic, msafara ulipita kwa mwendo wa taratibu katika njia panda ya Tazara na kuongeza kasi kuelekea mjini, walipofika njia panda ya Chang’ombe kitu wasichotegemea kilitokea, gari moja iliyokuwa ikielekea Magomeni kutokea Chang’ombe iliingia kwa kasi barabarani na kukatisha katikati ya msafara na kuigonga ubavuni BMW na kuisukuma pembeni, ile gari ya polisi ilisimama na kupiga rivas kabla ya kufika eneo la tukio polisi wale walisuka na bastola mkononi kuelekea eneo la ajali, vijana watatu walishuka kwa kasi kutoka katika gari ile iliyosbabisha ajali kuelekea ile BMW kabla hawajafika mmoja wao alipaishwa juu tayari kifua chake kilifunuliwa vibaya na risasi kutoka kwa polisi mmoja, kabla hawajatahamaki vijana wale walijikuta na wakati mgumu kidogo, polisi mmoja alifyatua risasi kumuelekea kijana wa pili lakini shabaha haikuwa nzuri kijana yule alijiviringa chini na kutoa shortgun kwenye koti lake na kupiga risasi ovyo zilizowatawanya askari wale yule wa tatu akafika katika BMW na kupiga ngumi kioo cha abiria wa nyuma ambako alikaa Bw. Chiwawa na kuinyayua briefcase ya Bw. Chiwawa, aliondoka kwa kukimbia na kumuacha mwenzake ambaye alipotaka kunyanyuka alipigwa risasi ya mguuni nakuanguka chini. Yule aliyebeba briefcase alipoona yuko matatani alikimbilia kwenye gari na gari ile ailigeuzwa`kwa mtindo wa hatari kuelekea Gongo la mboto.
Polisi waliendelea kuifukuza bila mafanikio.
Bw. Chiwawa hali yake haikuwa mbaya ila alikimbizwa hospitali ya taifa Muhimbili kwa matibabu. Ulinzi wa kutosha uliwekwa nje na ndani ya hospitali hiyo kila aliyeingia kumuona Bw Chiwawa alifanyiwa ukaguzi wa kina. 

Riyadh International Airport Saudi arabia
Boeing 747-400 Jumbo Jet ya shirika la Uingereza aliyosafiria Bw Chiwawa*******************
Dhaka-Banghladesh 


Kikao kizito kiliendelea huko Dhaka katika nchi ya Banghladesh katika hotel ya Nyota tano ya Hilton, hoja ilikuwa ngumu
“Tumekosea!” mmoja wa wajumbe aling’aka “ilitakiwa ile DVD alipomaliza tu kuangalia ichukuliwe sasa tumechelewa.” Aliongeza Bw Mahmoud Bashir
“Kwani ni nani alikuwa safarini?” mjumbe mwingine aliuliza
“Safarini tulimtuma mpiganaji namba 3 Bw Boniface Mc Field” alijibu mwanamama pekee aliyekuwa katika kikao hicho
“Inabidi tuwe makini sana, sasa cha kufanya ni kuhakikisha hiyo DVD inapatikana kabla haijaonekana na mtu mwingine” aliongeza mkuu wa kikao hicho Bw James Washington.
Kikao kiliendele na hoja nzito nzito zilijadiliwa, kuu ikiwa ni jinsi ya kupenyeza utawala wao katika taifa la Tanzania, kuwanunua wanasiasa maarufu na kuwapa pesa ili kujiweka vizuri katika uchaguzi ujao kushinda halafu wao kupitia viongozi hao kujinufaisha kwa rasilimali nyingi zilizopo nchini. Kutokana na hilo kamati iliundwa ya matajiri wakubwa kutoka pande mbalimbali za sayari hii. Tayari walikuwa wameshafanya hivyo katika nchi mbalimbali za Africa ambazo nyingi mpaka sasa zimeingia kwenye machafuko makubwa, mauaji ya kimbari na hata kupoteza thamani za utu kwa kupitisha miswada isiyostahili. Lakini jicho lao kubwa lilielekea katika nchi moja yenye utajiri mkubwa Africa ambayo bado ilikuwa na utawala imara usiotetereka, usioyumbishwa na mtu au taifa lolote liwe tajiri kifedha au kwa nguvu za kijeshi. Lakini kutoka na uchu wa kujilimbikizia mali kwa viongozi nchi hiyo basi na hawa jamaa wanaojiita ‘The SIXs’ ambao wana mtandao mkubwa duniani na wamejijenga katika nchi nyingi waliona sasa wanaweza kuingia katika nchi hii ambayo tayari kuna watu wapenda mali wawatumie ili kufanikisha lengo lao.

Kikao kilifungwa na kila mmoja alirudi katika shughuli zake za kawaida wakiwa wamekubaliana kukutana kwa kikao cha tatu uko huko Dar es salaam baada ya siku chache ili wakamilishe lengo lao.

********************
Mwanza City 


Amata Ga Imba aliendelea kula raha na mrembo wake Sundi, aliyekutana naye katika klabu ya usiku ya Sukuma Night Club ambako alienda usiku iliopita. Wakiwa kitandani wakifurahia maisha asubuhi ile huku wakiangalia TV ya taifa mara alisikia habari iliyomshtua na kumfanya kutoka kitandani na kuketi kuangalia

“...tukio hilo lililotokea asubuhi hii katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa kwenye mataa ya Chang’ombe, lilihusisha gari mbili mojawapo ikiwa ya Mh. Chiwawa Chakwima.Watu hao wasiojulikana  ambao walivalia soksi nyeusi usoni waliivamia gari ya Mh Chakwima na kupora briefcase na kutokomea nayo, polisi waliokuwa eneo hilo walifanikiwa kulipiga risasi jambazi mojawapo na kulitia mbaroni, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na Mh Chakwima yuko hospitalini kwa matibabu...”

Amata Ga imaba alipigwa na butwaa lakini hakutaka kuonesha hali hiyo kwa mrembo yule aliyekuwa naye asubuhi ile, alijinyanyua na kutaka kuelekea kibarazani, yule mrembo alimuwahi na kumvutia kitandani
“Unaenda wapi mpenzi mi nakuhitaji hapa!” alijisemesha kwa sauti ya kubana pua na kumpa Amata busu la kinywani, bila kujali waliendelea kupeana mahaba mazito, mara mlango uligongwa lakini wawili hawa waliendelea na malavidavi yao wakiwa kwenye kilele cha mahaba, mlango uligongwa tena, Sundi alitaka kwenda kuufungua lakini Amata alimzuia kwa kumbana barabara, mara ya tatu mlango uligongwa na kimya kikachukua nafasi yake, moja kwa moja Amata alielekeza macho yake chini ya mlango na kuona bahasha ya kaki iliyopenyezwa hapo, akaamka na kuifuata akaichukua na kuifungua ndani akakuta simu ya maneno Telegram

 “rudi nyumbani haraka mama ni mgonjwa mahututi anakuhitaji Tena Sana Aisee.”

Amata alishaelewa mara moja ujumbe huo maneno yaliyokaziwa kwa herufi kubwa ndiyo yaliyomfanya ajue simu ile ilitoka wapi... “Tena Sana Aisee” ... simu yoyote iliyomaliziwa na maneno hayo ilikuwa ni ya haraka na yenye uzito mkubwa. Amata aliiweka karatasi ile mezani na kuingia bafuni haraka akaoga na kuendelea na maandalizi ya chapchap, ndani ya dakika kumi alikuwa ameshajikamilisha akiwa ndani ya suti ya buluu na tai yake iliyomkaa vizuri
“mbona hivo dia kumetokea nini?...” Sundi aliuliza, Amata alimrushia ile karatasi kitandani
“Ha! Ina maana unaenda Dar sasa? Pole mpenzi, mpe pole mzaa chema” Sundi alisema hayo baada ya kuisoma simu ile ambayo yeye hakuielewa hata kidogo. Amata alifungua walet na kumpatia noti nyekundu tano, akachukua briefcase yake tayari kwa safari
“Mpenzi! Asante kwa kampani ngoja niwahi nyumbani nitarudi baada ya siku chache tumalizie raha zetu” akamwachia  na busu nene na kutoka chumbani.
Ndege ya shirika la ndege la Tanzania Boeing ilikuwa tayari kuondoka lakini kutoka na na ujumbe walioupata ilibidi wasubiri kidogo, Amata alifika uwanja wa ndege na moja kwa moja akachukua usafiri... hakuna maswali! Ndege iliiacha ardhi ya Mwanza na kukata anga kuelekea Dar yapata saa mbili na nusu asubuhi. Muziki laini wa congo ulikuwa ukisikika katika chombo cha kusikilizia muziki katika ndege hiyo, akiwa kwenye wimbi la mawazo kupanga na kuoangua kwa kuwa alijua anachoitiwa ni kitu gani, muziki ule pia ulimrudisha mbali sana aliamkumbuka rafiki yake wa shule ya msingi Bw Namoto Arap Manda ambaye kwa wakati huo naye alikuwa na majukumu mazito katika Taifa.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa Dar es salaama alikuwa akisubiriwa, mara moja aliingia katika gari na kuelekea mjini... kazi imeanza!
Ndege ya ATC aliyotumia Amata Ga Imba kusafiri kurudi Dar kutokea Mwanza


Je Amata Ga Imba ni nini ametiwa Dar es salaam?
Kama umevutiwa na kipande hiki cha hadithi hii.... comment uone kitakachoktokea...

Monday, January 14, 2013

MSITU WA SOLONDO


MSITU WA SOLONDO

Mtunzi:Amata Ga Imba


“3”Sehemu iliyopita...
Tuliona Amata kakimbia ghafla huku wenzake wakishindwa kujua kapatwa na nini, JE Amata alirudi au La?
Endelea kupata uhondo huu... unaruhusiwa kutuma comments zako juu ya simulizi hii kama iendelee au iishie hapa.

Walibaki kujadiliana tu nini cha kufanya kwa kuwa hawakujua Amata kaenda wapi na kwa nini. Wakiwa katika butwao hilo mara walisikia kelele za mnyama mwenye hasira kutoke porini wakiwa bado hawapo vizuri mnyama aina ya Ngiri alikatiza kati kati yao kwa kasi ya ajabu alimpiga, Bw Stephan alipigwa kikumbo na kudondoka vibaya kwenye mawe bunduki ikianguka upande mwingine, wengine wlikimbia kila mtu upande wake wakiwa wamechanganyana hawaelewi kilichotokea. Bw Stephan aliumia sehemu ya mkono alikuiwa akivuja damu. Amata akasimama mbele yao
“nauliza tena! Nyi mnaweza kuingia Msitu wa Solondo? Huyo ni ngiri tu mmekimbiana hivyo wengine na bunduki zenu mmeshindwa kujipanga kumshambulia, sijui kama tutarudi mi nina wasiwasi.” Amata aliwaeleza huku akitweta.
“Amata acha ujinga!” Saringo aling’aka
“Sio ujinga mimi nilienda porini kumkurupusha huyo mnyama ili niwapime uwezo wa kukabiliana na hatari za ghafla, maana huko msituni kuna wanyama wakali, na isitoshe kuna mashetani ambayo hata uyaoni kwa macho we utahisi unatandikwa bakora tu! Sasa itakuwaje?” Amata aliwauliza kwa ukali
“Haya na tuanze safari mengine tutayaona uko huko!” Saringo aliwaambia wengine.

Safari ya kuingia Msitu wa Solondo ikaanza, Golan akiwa na jisu kubwa kiunoni mwake aliongoza msafara akifuatiwa na Bw. Stephan na bunduki yake kubwa, Saringo akiwa na begi lake la kijeshi mgongoni alionesha kutembea mwendo wa kikakamavu haswa, Bi.Hellen mkimya asiye na maneno mengi aliendelea kuchapa mwendo na bastola zake kiunoni alionekana amejiandaa haswa katika safari ile ngumu. Walipita katikati ya msitu ni ndege na wadudu ndio waliokuwa wanawasindikiza, Amata akiwa na uta wake mgongoni alikuwa wa mwisho katika msafara huo ambao ulikuwa ukiongozwa na Golan hakukuwa na anayeongea kwa wakati wote huo, walikuwa wakifuata kajia kadogo kanakoelekea milimani, ilionekana kuwa Golan alikuwa mzoefu wa eneo hilo kwa kiasi fulani ukiacha Saringo ambaye aliku na karatasi kubwa tu la khaki ambalo ndani yake kulikuwa na  michoro mingi ya ajabu na isiyoeleweka. Amata akiwa hana wasiwasi nyuma ya wote alivuta hatua uku akiwa na mgagi wake mdomoni, baada ya mwendo mrefu wa kama masaa matatu hivi walifika mtoni ambako ilibadi wavuke kwenda ng’ambo ya upande wa pili, maji ya mto yalikuwa yanakwenda kwa mwendo wa wastani, maji haya yaliyochanganyika na udongo yalikuwa na rangi kama chai ya maziwa.
Wote walisimama kando ya mto huo wakiyaangalia maji kwa makini
“Inabidi tuvuke!” Saringo aliwambia wenzake. Wote wakatazamana na kuanza kujiandaa kwa kuvuka hakuna aliyejua kina cha mto huo wala hatari yoyote iliyopo hapo, hakuna aliyeonekana kuogopa bali kila mtu alionesha ujasiri, Amata alionekana kasimama tu kana kwamba hakuwa mmoja wao katika hilo.
“Kuna kamba? Inabidi mmoja aogelee mpaka ng’ambo akafunge hiyo kamba kwenye mti ili wengine iwe rahisi kuvuka” Amata alitoa rai. Na kila mmoja kukubaliana na wazo hilo. Stephan akatoa kamba ndefu ya kutosha Golam akajitolea kuivusha kamba hiyo. Akaichukua na kujifunga kiunoni tayari kwa kuvuka, aliyaangalia yale maji kwanza kisha akachukua podo na uta wake na kuuweka mgongoni tayari kwa kuvuka
“Naomba mnilinde” Amata aliwaambia wenzake na kujitoma ndani ya maji aliogelea kwa ustadi sana kukatisha mto huo, maji yalikuwa magumu kwake katika kuvuka. Alikotoka wote walikuwa kimya kumuangalia Amata jinsi anavyoyakata maji japo si kwa ustadi sana wakiwa bado katika kumwangalia mara walimuona Amata akizama kabla hawajajiweka vizuri waliona mkia wa mamba mkubwa ukitokeza juu ya maji
“Mamba!!!” Golam alipiga ukelele. Amata alibanwa mguu na mamba alijitahidi kujinasua lakini mamba yule alimzamisha tena, aliipomuibua mara ya pili alichomoa mshale mmoja kutoka katika podo lake na kumchoma mamba yule jichoni, Mamba alimuachia Amata na akajigeuza chali Amata kwa ustadi mkubwa alimchoma tena eneo la kifua mamba yule kisha akajaribu kuogelea kwa kujihami, mamba yule akajinyayua juu Bwana Stephan kwa ustadi mkubwa alimlenga na kumpiga risasi mbili eneo la tumbo mamba yule alijibwaga majini... mfu!. Bw Stephan akashusha bunduki yake na kushusha pumzi ndefu, Amata alifika ng’ambo na kuifunga kamba ile mtini kisa kuwapa ishara wengine kuvuka, mmoja baada ya mwingine walivuka na hatimaye wote walifanikiwa kuvuka. Bi Helen aliuangalia mguu wa Amata lakini haukupata majeraha makubwa alipohakikisha kuwa anaweza kusonga mbele basi safari ikaendelea. Giza lilianza kuunyemelea msitu
“Hapa tunaweza kulala” Amata alilisisitiza wakakoka moto na kupumzika. Kila mtu akiwa amejilaza kwa mang’amung’amu. Saringo alilala jirani kabisa na Amata, Hellen akiwa jirani na Stephan, Golam alikuwa mbali kidogo kakaa kaegemea mti peke yake. Usiku mnene ulifika msitu wote ulitulia, moto uliendelea kuwaka polepole, Golam alinyanyukla pale alipo na kuja kwa wenzake
“Amata!” akamuamsha Amata kwa upole Amata akaamka, Golam akamuonesha ishara ya mkono kuangalia upande wa pili, Amata aliona wasichana wawili kwenye kamfereji wakiwa kama walivyozaliwa, weupe, warembo wana nywele ndefu. Wakiwa wanatazamana macho na wasichana wale, mara wale wasichana wakaanza kuwaita kwa ishara ya mkono, Golam alichanganyikiwa akiwa kasimama wima mwili wake ukionekana wenye hitaji baada ya kukaa gerezani miaka sita bila kuona hata utupu wa mwanamke alivutiwa na wasichana wale hata kusahau kila kitu na kutamani kwenda. Amata aliwaangalia kwa makini, akili ikamrudia ghafla ‘msituni hapa wasichana hawa wametokea wapi?’.
“Golaaammmm” Amata aliita kwa nguvu, ukelele uliowaamsha wengine, Golam aliendelea kuelekea kwa wale wasichana huku akianza kuvua nguo zake, Golam aliwafikia wale wasichana nao wakamdaka na kuanza kufanya mapenzi, kelele za mahaba zilisikika kwa nguvu hata zikageuka kuwa kelele za kutisha za wanyama wa ajabu lakini pale walipokuwepo hapakuonekana mtu tena.

**************

Je ni nini kimemtokea Golam?
Wale wasichana walitoka wapi? Ni akina nani?

Usikose kusoma sehemu ya nne ya simulizi hii Msitu wa Solondo...

Monday, January 7, 2013

Sehemu ya pili "MSITU wa SOLONDO"
MSITU WA SOLONDO
"2"

Mtunzi:Amata Ga Imba


Ilipoishia wiki iliyopita:

Amata na Golam wamefanikiwa kutoroka kutoka gereza la Saroge kwa kupitia njia ya siri. Baada ya misukosuko mingi ndani ya maji wamefanikiwa kutoka salama na kukutana na Saringo pamoja na wazungu wawili. Je; ni nini wanakitaka kutoka kwao?

Jiunge na msimulizi wako Amata Ga Imba katika simulizi hii ya kusisimua... drop ur comments.

Msitu wa Solondo ni msitu mkubwa wenye miti mingi na wanyama wakali, ndani yake wanaishi watu wa jamii mbalimbali wenye mila tofauti za kizamani. Watu wengi waliuogopa msitu huo kutokana na kile kilichosemwa kuwa kuna miujiza mingi, uchawi na hatari za kila aina pia waliamini kuwa majini na mashetani hutokea katika msitu huo. Msitu huo ambao wakoloni wa kijerumani na kiingereza walihifadhi mali nyingi sana uliachwa katika hali hiyo hakuna hata aliyediriki kuingia baada ya kusikia kuwa wapo waliojaribu kwenda huko hawakurudi wengine waliliwa nyama na kupotelea huko. Kwa hiyo kila mtu aliogopa hata kuzungumzia. Matambiko na ibada za kijadi zilifanyika katika msitu huo, katikati ya msitu huo kulikuwa na jiwe kubwa sana jeusi ambalo kwa kuliona tu linatisha na inasemekana lilikuwa linaongea, hapo ndipo walipotolea sadaka ya damu jamii walioishi ndani ya msitu huo. Katika jiwe hilo kulikuwa na pango kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na mapango madogomadogo mengi, jamii iliyokuwa inaishi katika msitu huo ambayo iliitwa ‘Gorino’ , gorino kwa lugha yao ilimaanisha ‘mla watu’ walikuwa wanawakamata watu wanaoingia ndani ya msitu huo na kuwaficha katika pango hilo ambalo wao waliamini lilikuwa ndio nyumba ya Mungu wao na kila walipotaka kutoa sadaka walichukuwa mmoja wa watu hao na kutoa sadaka ya damu, waliwakata vichwa na kuwatoa kafara, nyama iliyobaki ililiwa na vichwa vilining’inizwa kama mapambo ya eneo hilo hii ilikuwa ni sherehe kubwa sana ngoma zilipigwa na walicheza, hakuruhusiwa mwanamke kusogea hapo kwani waliamini mwanamke atamkasirisha mungu wao. Lakini eneo hili ambalo wakoloni walilitumia kama hifadhi ya mali zao lilikuwa ni lasiri sana kiasi kwamba hata wakazi wa huko na pembezoni hawakujua ukweli huo, madini mbalimbali yaliyohifadhiwa pangoni humo miaka ya elfu moja mia nane hamna aliyeyagusa kwa kutokujua, Msitu huo ulibaki katka hali niyo watu weupe wengi walijaribu kuingia kwa kuwa walijua ni nini kipo huko lakini nao waliishia uko huko.

Amata alirudiwa na fahamu, akiwa pale chini bado alitazama juu na kuona watu watatu kati yao alimtambua Golam ambaye alichuchumaa jirani yake pembeni yake kulikuwa na mwanaume mwingine mwenye asili ya kizungu ambaye hakumjua alimuona mwanamke mwingine naye alikuwa na asili ya kizungu, Amata alizidi kuchanganyikiwa kwani hakuwajua hao wote ni akina nani, ghafla alipata mshtuko ambao ulimfanya anyanyuke ghafla na kushikwa na mshangao kwa kumuona huyu aliyesimama mbele yake sio mwingine ni Saringo. Huyu alimtambua bila kificho kwani kati ya wote huyo ndiye aliyemfahamu kwanza, Amata aliwatazama wote mmoja baada ya mwingine ila alimkazia macho sana Saringo ambaye bado alikuwa hamuelewi uhusiano wake na matukio yote haya.
“Amata, kaa chini tuongee kidogo...” Saringo alimuomba Amata. Amata akaketi na wengine wote wakafanya hivyo. Wakiwa wamezunguka moto uliokuwa unawake hapo alfajiri hiyo ili kuidhibiti baridi kali iliyowanyanyasa, kando yao miti mirefu na mikubwa iliwazunguka, mto mkuwa wa maji mengi yaendayo kasi ulipita eneo hilo, kelele za ndege wakubwa zilisikika.
“Hawa unaowaona ni rafiki zangu, huyu anaitwa Bw. Stephan Van Leuwen kutoka Poland na huyu ni rafiki yake kutoka German anaitwa Bi. Hellen Schurman wote ni wakufunzi katika chuo kikuu cha Heidernburg huko Ujerumani, ni wataalamu wa mambo ya kale. Huyu mwengine unamfahamu Golan, huyu ni binamu yangu mtoto wa mjomba wangu, na mimi naitwa Saringo mjukuu wa mzee Koloto.” Saringo alitoa utambulisho huo, kisha akageukia upande wa pili
“Huyu anaitwa Amata!” alimtambulisha kwa kifupi
“Amata Ga Imba, au mate ya Simba” Golan aliongezea na wote wakatabasamu
Amata bado alimkazia macho binti huyu anayeitwa Saringo ambaye alionekana mkakamavu akiwa ndani ya jinsi iliyomkaa vizuri na fulana yake nyekundu ambayo kwa nje aliifunika na kishati cha buluu angavu ambacho hakufunga vifungo ila alifunga fundo kwa chini, buti kubwa nzuri ya kijeshi aliyoitupia mguuni mwake haikuwa ya kawaida. Amata bado alikuwa hajaelewa vizuri kinachondelea hapo alipomtazama yule mzungu ambaye kichwani mwake alivaa kofia kubwa kama ile ya Marlboro akiwa anavuta kiko yake, mgongoni akiwa na begi la kijeshi na mkononi akiwa na bunduki aina ya ‘rifle’, na rafiki yake wa kike mwenye macho makali daima litafuna jojo akiwa kavaa jinsi ya kaki na shati zito pia la kaki, alionekana mtaratibu na mpole kiunoni mwake alikuwa na bastola mbili kushoto na kulia. Amata aliogopa sana kwakuwa kwanza alizoea kuwaona wazungu makanisani tu na wakiwa wamevaa makanzu, alizoea kuona bunduki za kuwindia tu kama gobole ambalo hata yeye aliachiwa na marehemu baba yake. Alikuwa na mawazo mengi yaliyokuwa yakipita kichwani mwake.

“Tuko hapa kwa nia moja tu, tunakwenda ndani ya msitu wa Solondo, sisi watano na wewe tuliona unatufaa, mimi ndiye nilikutafuta kwa gharama kubwa” Saringo alimuambia Amata. Amata akaendelea kumsikiliza kwa makini, Saringo akaendelea
“Nilikuja kijijini kwenu kumsalimia shoga yangu Chausiku ambaye unamfahamu sana, nikiwa pale ule ugonvi uliokuhusisha wewe niliuoana na nilivutiwa kwa jinsi ulivyompa mkong’oto yule bwege. Nikafuatilia mwisho wake kuona, nilipojua kuwa umekamatwa na uko polisi nikaja kukutembelea nilikuja tu kukutia hasira na si kingine lakini nilipanga wewe ufungwe nikiwa na lengo moja kuwa kule gerezani utakutana na binamu yangu Golam na kweli ikawa hivyo, Golam nilimpa kazi muda mrefu ya kutafuta mfungwa mkakamavu, mpiganaji, asiyeogopa kitu na ulivyofungwa wewe nikamwambia Golam akuchunguze, siku chache tu akanipa taarifa nzuri ya kuwa ulimpiga hata mtu ambaye wao wote wanamuogopa, ndio hapo tukasuka mpango wa kukutorosha wewe na Golam, na mpango huo tuliusuka mimi na hawa wazungu kwa kuwa sisi tulikuwa na ramani ya gereza lile, njia zote za siri ambazo wenyewe wakoloni walizitumia kuwakimbia maadui pindi wanapovamiwa.” Saringo akakohoa kidogo na kuendelea
“Baba wa babu yangu alifanya kazi kama askari wa mkoloni na kituo chake kilikuwa hapo gerezani, wakati huo ikiwa ngome ya mjerumani kabla ya kuchukuliwa na waingereza, yeye ndiye aliiba hii ramani, yeye pamoja na wenzake ndio walikuwa wanaenda Solondo kuhifadhi vitu vingi vya wajerumani, alimpa babu yangu siri hii miaka mingi sana mpaka kwa baba yangu, baba yangu alinipa siri hii na kabla ya kufa kwake alifuatwa na watu wengi sana waliodhani kuwa yeye alikuwa anajua zaidi na amefika huko katika pango la msitu wa Solondo. Kabla hajafa alinipa mkoba wake mchafumchafu nilipoufungua ndani ndio niliona makaratasi ya kizamani na maandishi ya ajabu ajabu siyaelewi, nilihifadhi karatasi zile vizuri, na nilipokwenda masomoni Ulaya ndipo nilikutana na hawa rafiki zangu katika darasa moja, nilipojua vizuri kijerumani ndio nilipojua maana na siri nzito iliyomo katika makabrasha yale, ndio hapo tulipopanga kikosi kazi kuukabili msitu huu wa Solondo hadi tuone mwisho, tukaona wewe pia unafaa kuwepo katika kikosi kazi hiki”.
Amata alibaki ameduwaa ‘Msitu wa Solondo!’ alijiwazia aliona kama yuko katika ndoto labda ataamka lakini haikuwa hivyo.
“Saringo!” Amata aliita na kuweka pozi kabla hajaendelea kuongea “unaujua msitu wa Solondo au umeusoma tu kama ulivyosema?”
“Sijawahi kuingia msituni ila sasa tumeamua kwenda” Saringo alimueleza Amata
“Msitu wa Solondo sio wa kuuchezea, tutakufa sote hakika, kuna mashetani na viumbe vya ajabu, kwa nini tuyakatishe maisha yetu tukiwa bado vijana? Kuna nini kule cha maana? Acheni upumbavu wenu. Golam ndio hii safari uliyotaka twende?” Amata alimuuliza Golam.
“Amata! Hii ndiyo safari, usiogope zile ni hadithi tu, wazee hawakupenda twende huko lakini ni msitu tu wa kawaida. Ujue kila kona sasa unatafutwa mfungwa uliyetoroka utajificha wapi? Twende Solondo” Golam alijibu na kutoa tabasamu lake la kuvutia ambalo daima humfanya Amata kucheka.
“Hao wazungu wanaweza kutembea kwa miguu? Maana ni safari ya siku kama saba hadi tufike.” Amata aliuliza kwa wasiwasi
“Wataweza ndio maana wamekuja.” Saringo alijibu
Amata akatikisa kichwa kuashiria kuwa ameridhika, akanyayuka akaingia kwenye vichaka vya karibu akatokomea huko. Saringo, Golam na wenzao walibaki kumsubiri bila mafanikio.

Je Amata amekwenda kufanya nini?
Je Amata atarudi tena au la?

Usikose kusoma sehemu inayofuata?

Thursday, January 3, 2013

MSITU WA SOLONDO


safari ya hatari ya Amata Ga Imba
 
MSITU WA SOLONDO

Mtunzi:Amata Ga Imba

Amata Ga Imba aliendelea kunywa kahawa yake polepole kana kwamba hana shughuli nyingine ya kufanya kwa siku hiyo, kichwani akiwa na mawazo mengi sana akipanga na kupangua juu ya maisha yake ya sasa na baadae, alipotahamaki hata kashata alizokuwa akila zilikwisha moyoni akajiuliza kama aliagiza kashata au ameshazila zimekwisha! Hilo nalo likawa jambo jingine ambalo lilikosa jibu kabisa.
“Chausiku!!” aliita kwa nguvu kana kwamba aliyekuwa anamuita alikuwa umbali wa kilomita kadhaa lakini kumbe wote walikuwa hapo jirani tu.
Watu walishtuka kwa sauti hiyo hata wengine walidiriki kumtupia maneno yasiyostahili
“Samahani waheshimiwa!” aliomba msamaha
“Samahani nini mjinga wewe!” mmoja alitamka kwa hasira
“Wengine tuna BP utatuuwa bure sura ka Sokwe!” mwingine aliongeza
Amata aliumia sana moyoni kwa tukio lile, akainamia mezani, akatikisa kichwa kisha akasimama kwa hasira na kuelekea eneo la kunawia mikono, akajitazama kwenye kioo, akatabasamu, kisha akageuka na kurudi alipoketi kwanza.
Kabla hajaketi alisikia sauti nyuma yake
“Umejiona ee? Ka sokwe, tena wa Gombe!” mmoja alimkejeli, wengine wakaangua kicheko cha dharau na kupiga miluzi.
Hasira za dharula zikamrudia Amata, akageuka na kuelekea upande ambao sauti ile imesikika
“Nani aliyesema vile?” aliuliza kwa kung’aka, wakacheka tena
“Ukimuona utamfanya nini? Fala wewe mtoto wa porini!!” mwingine alisema na wengine wakaangua kicheko. Amata alipiga hatua mbili mbele na kumkunja shati yule aliyesema maneno hayo akamuinua kwa nguvu akamrusha chini, huyo akaanguka chini mzimamzima kama gunia, jamaa akanyanyuka kwa hasia na kumvamia Amata, Amata akamdaka na kupiga vichwa vitatu vya nguvu akamsukuma kidogo na kumrushia makonde kama mvua, kijana yule alichanganyikiwa hata hakuweza kujibu mashambulizi alianguka chini mara ya pili.
“Ameua! Ameua! Ameua!” kelele za watu zilijaza mgahawa ule mara watu wakajaa wanataka kumshika Amata. Yule kijana bado alikuwa chini hajitambui kwa kipondo cha ghafla alichokipata. Amata aliruka kutoka aliposimama akatua juu ya meza na kutaka kutoroka kwa kupitia dirishani, watu walimgombania kwa kumshika shatia wengine suruali, masikini Amata shati lake lilichanika vibaya akabaki na fulana ya ndani na kuwaachia shati wananchi wenye hasira, alliruka kupitia dirisha la mgahawa huo na kudondokea kwenye lundo la mawe kwa kutanguliza mkono, alihisi maumivu makali ya mkono lakini alipogeuka aliona watu wale wanakuja pale alipo, akanyanyuka na kutimua mbio
“Huyo huyo! Kamata muuaji huyo!!” kelele za wananchi wale zilikuwa kama kichocheo kwa kijana Amata kuongeza spidi. Mara kwa mbele aligongana na pande la mtu na kuangushwa mbali, alinyanyuka na kuanza kukimbia tena, watu walitoka majumbani na kumuunganishia kama kawaida ya wananchi. Mbio ziliendelea na wananchi nao hawakuchoka, alitokea kwenye wigo wa nyumba la! Hapakuwa na njia aliruka na kupanda ukuta kisha akatokea upande wapili na kupanda tena alitua chini kwa miguu yake mikakamavu na kutimua mbio lakini la haula! Alipokuwa akijaribu kuvuka kichaka kidogo katika eneo hilo alijikwaa vibaya na kuanguka chini, mchezo umekwisha. Watu wakamkamata na kuanza kumpiga hata kumuumiza vibaya, Mungu si Athumani polisi waliwahi kumuokoa kutoka kwenye mikono ya watu wenye hasira.
“Tuachie huyo tummalize! Muuaji huyo!” watu walipiga kelele na wengine bado walidiriki kurusha hata mawe ambayo baadhi yaliwapata askari wale. Askari mmoja akafyatua risasi hewani na watu wale wakatawanyika kwa woga wakikimbia uku na huku wengine wakianguka na kukanyagana vibaya. Amata alichukuliwa mpaka kituo kidogo cha polisi akiwa hatamaniki kwa jinsi alivyolowa damu hata fulana yake aliyobaki nayo baada ya kuwaachia shati watu wale haikujulikana kama ni nyeupe au nyekundu, juu ya jicho lake la kushoto jeraha kubwa lilikuwa bado linavuja damu, mkono wake umevimba, kucha ya kidole gumba cha mguu wa kushoto haikujulikana hata imeng’okea wapi. Askari wale walimpiga Tanganyika jeki bila huruma wala kujali kuwa mwenzao ameumia namna ile wallimkokota tena na makofi juu mpaka kituo kidogo cha polisi na kumlundika selo. 

Ndani ya chumba kidogo cha selo katika kituo cha polisi cha kijiji wahalifu walijazana mpaka hewa haikutosha kabisa, walichoka na hata wengine kukosa nguvu, kupoteza fahamu kwa kukosa hewa ya kutosha. Amata aliingia kwenye selo hiyo katika hali ile aliyokuwanayo, akakaribishwa na joto na harufu mbaya haja kubwa na ndogo zilizochanganyika, mwanga hafifu uliopita katika kadirisha kadogo kenye ukubwa wa mlango wa banda la njiwa ndio pekee kalikokuwa kanatoa faraja kwa binadamu hawa waliokuwa na makazi ya muda ndani ya chumba hiki, wote walikuwa na sura za kutisha ambazo bila kuuliza utajua kuwa sasa nimeingia kuzimu.
Ucku huo ulikuwa mrefu sana kwa Amata, mawazo mengi yalitawala kichwa chake, maumivu makali yaliusumbua mwili wake, alijituliza kimya kwenye moja ya kona za kijichumba hiko huku akisikia kichefuchefu kama mama mjamzito kila mara alitamani kutema mate lakini atatemea wapi watu wamejazana hata wengine wamekaa kwa kupakatana mh!  Mawazo yaliendelea kumsonga hata usingizi mwepesi uliokatishwakatishwa kwa nyimbo za kuchukiza za mbu masikioni mwake ulikuja na kuondoka, aliwaza jinsi anavyoishi kwa shida hana baba hana mama, kula yake ya wasiwasi aliona jamii yote haimtaki, dunia imemchukia, ulimwengu unampa adhabu,
“Kwa nini mimi?” alijiuliza uliza moyoni mara kwa mara hata alipokuwa kwenye kibanda chake huko shamani kwao ambako alipitisha maisha yake ya ujana tangu wazazi wake walipofariki yeye akiwa na umri wa miaka kumi na tano, mama yake alikufa kwa kuliwa na simba na baba yake alikufa akiwa anamuokoa mama yake dhidi ya simba hao wenye njaa na uchu wa nyama ya binadamu. Kila aliporudiwa na picha hii alilia sana na kujiona kuwa yeye ni binadamu mwenye mkosi, akuwahi kuwa na kaka wala dada isipokuwa ndugu tu ambao pia hawakuwa na msaada nae kabisa.
“Amata!!!” aligutushwa na sauti kali ya askari iliyotokea kwenye kadirisha ka mlango wa selo hiyo.
“Afande!” aliitikia kwa uchovu na kujaribu kujiinua kutoa alipokuwepo lakini alijikuta anapata kizunguzungu na kuwaangukia wenzake waliokuwa hapo. Alifika mlangoni pale kwa shida mbele yake alimuona msichana mrembo sana kasimama, mrefu wa wastani maji ya kunde, alivalia vizuri suruali yake ya kitambaa nyeusi na blauzi yake nyeupe huku shingoni kafunga skafu yenye mchanganyiko wa rangi, nywele zake fupi zilizokatwa kiumahili na vinyozi wanaojua kazi yao, kiatu chake kirefu kilimfanya aonekane kuwa ni mrembo anayetunzwa na pedeshee fulani. Dada yule alijivuta taratibu mpaka kwenye dirisha lile. Amata alipokea pumzi safi iliyonukia na kuvutia kutoka kwa mrembo huyo, hakuamini anachokiona ni malaika au binadamu, aliduwaa, akapigwa na bumbuwazi, mikono yake ikiwa imeshika nondo mbili zenye kutu alijikuta anaishiwa nguvu. Mrembo yule alishika nondo zile kwa kubana mikono ya Amata akaiangalia sura ya Amata iliyochoka na kukaukiwa na damu..
“Saringo! Naitwa Saringo” almwambia Amata kwa sauti ya chini
“Hunijui, ila utanijua punde tu” aliendelea “Haujaua ila umeumiza vibaya, sasa unastahili zawadi kwa kazi uliyoifanya bila kujua, na zawadi hiyo utaipata ukimaliza kazi yako” Saringo alishusha pumzi na kumwangalia Amata usoni na kumuona jinsi alivyochanganyikiwa, akaendelea kumwambia mashairi yake yasiyoeleweka kwa mtu mwenye akili timamu, sasa kwa kukunja sura akamwambia Amata “ Lazima ufungwe, uishie jela!” akageuka nakuondoka zake. Amata akazidi kulowa jasho, maswali yasiyo na majibu yalimzunguka tena ‘nilijua malaika mwema kaja kuniokoa kumbe malaika mbaya wa mauti kanitembelea’ alijiwazia na kuanza kulia. Amata hakupata jibu mwanamke yule ni nani, na anataka nini, utata. Asubuhi ile kalandinga liliwachukua mpaka mahakama ya kijiji, jalada la Amata lilikuwa la tatu kuitwa, taratibu akiwa na pingu mikononi aliingizwa katika chumba cha hakimu na kusomewa mashitaka ya kudhuru mwili, alijikuta hana cha kukana isipokuwa kukubali, kesi ikahairishwa mpaka baada ya siku kumi na nne. Walipokuwa wanarudi kwenye kalandinga alimuona binti yuleyule akiwa amesimama katika kundi la watu waliokuja mahakamani hapo, muonekano wake ulikuwa tofauti na wote pale kwani ndiye aliyevaa nadhifu kuliko wote ‘huyu ni nani?’ Amata alijiuliza hakupata jibu, moyoni alimlaani kuliko anavyomlaani shetani walipogongana macho Amata alitema mate chini na kumuonesha kidole cha kati. Mara alijikuta anatandikwa kofi la kisogoni au vijana huita ‘mbata’
“Panda juu unatuchelewesha!” sauti kali ya askari ilisikika. Amata na wengine wakapanda na lori lile kuondoka kwa kasi.

*************

“Una mpenzi mzuri sana, mtoto kaumbika kama Malaika, he he he mbona wewe na yeye hamuendani kabisa au wewe ni mchunga ng’ombe wao!” mmoja wa mahabusu alimuuliza Amata kwa sauti mbaya ya kukwaruza isitoshe inatisha. Amata aligeuka na kumwangalia akatabasamu kwa sura iliyochoka
“Simjui hata anatoka wapi” alimjibu
“Kwangu ni kama shetani tu yule, anataka kuniua, kunifunga, hilo ndilo limemleta hapa” aliendelea kumueleza yule mahabusu.
“Kwa nini aje kukuona asubuhi yote ile? Au kuna uhusiano wowote na kesi yako?” aliendelea kudadisi mahabusu yule, “Sijui chochote! Mbona maswali mengi umempenda? Mfwate basi, mi nshakwambia smjui! Yule ni shetani tu” Amata alijibu kwa hasira kidogo na mahabusu yule hakuendelea na maswali yake.

Kesi ilitajwa tena baada ya siku kumi na nne, Amata na wenzake wakiwa na pingu mikononi waliingizwa katika chumba maalumu cha mahabusu mahakamani hapo, Amata alisimama karibu na mlango, mara ghafla alipata mshtuko mkubwa, hakuamini alichokiona nje ya jingo hilo, akakaza macho kutazama kwa makini akayafikicha kidogo aone labda alikuwa ndotoni lakini hapana alichokiona ni sahihi na macho hayakumdanganya. Hakutaka kupoteza hata sekunde katika lile alilokuwa anliona lakini bahati mbaya hakuweza kusikia kinachozungumzwa. ‘Yule sio Chausiku?’ alijiuliza moyoni lakini pia hakutaka kuyaamini macho yake.

Chausiki Binti Saidi, msichana mfupi mwenye afya njema kibonge, mmiliki wa mgahawa unaojulikana kwa jina la Chau Café, msichana huyu ambaye amekuwa pamoja na Amata, wamesoma shule moja ya msingi kijijini hapo na kucheza michezo mingi ya utoto pamoja, yeye alifanikiwa kufika japo darasa la saba wakati Amata alifukuzwa shule akiwa darasa la tano kwa kisa cha kumpiga mawe mwalimu wake wa darasa. Maisha yalimwendea kombo Amata lakini Chausiku ndiye alikuwa akimfadhili japo kwa hela ya sigara au kikombe cha Kahawa, watu walikuwa wakimbeza sana Chausiku kwa jinsi alivyoonesha upendo kwa Amata hii ikapelekea Chausiku kutokuwa karibu sana na kijana huyu ambaye japo alikuwa mchafu, mkorofi lakini moyo wake ulituama kwake kama maji yatuliavyo mtungini yasipoguswa. Vijana wengi walipenda kwenda mgahawani kwake japo tu roho zao zisuhuzike kwa kumuona binti huyu, wapo waliomdanganya kwa pesa na vitu mbalimbali lakini msimamo wake thabiti haukumfanya ayumbishwe na vitu vyote hivyo bali aliuacha moyo wake utue kama kipepeo atuavyo katika ua alilolichagua. Chausiku aliumizwa sana na kisa kilichomkuta Amata, alijua kuwa Amata kwa hali aliyonayo asingeweza kupata msaada wowote wa kisheria au utetezi katika kesi yake, alijitahidi kufanya kila awezalo ili tu amsaidie Amata katika hili.

Jalada la Amata liliitwa, polisi walimtoa katika chumba kile akiwa chini ya ulinzi na kupelekwa katika chumba cha mahakama, akiwa anapita katika kikorido kidogo cha jengo hilo alisikia sauti nyembamba tamu ikipenya masikioni mwake, ilikuwa si ya mwingine bali Chausiku ambaye alikuwa akilia kwa machozi mazito “Mnyezi Mungu akusaidie” ni maneno aliyomwambia, Amata aligeuka kwa kuiba, alifarijika kuona kumbe wapo katika binadamu awa hawa wanaompenda, kidogo alijisikia mtu kati ya watu.
 Kesi ya Amata ilikwisha alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na miezi sita jela. Waliondolewa mahakamani na Amata alianza kutumikia kifungo chake huko gereza la kilimo Sogera, gereza lenye kazi ngumu, kulima, kupanda, kuvuna, muda wote mkiwa katika matope, maji machafu, mnakula chakula huku mnanyeshewa na mvua, mateso!.

Sogera ni gereza kubwa sana lililoko nje kabisa ya mji wa Mgosola, lilijengwa zamani na wajerumani wakoloni juu ya mlima. Limezungukwa na ukuta usiopungua mita ishirini kwenda juu na chini ya ukuta huo kumepandwa mikonge kuzunguka gereza zima, katika kona zote na katikati ya pande zote kuna vibanda vipatavyo nane juu kabisa vyenye walinzi wawiliwawili kila kimoja wakiwa na silaha kali, juu ya ukuta kumezungushwa waya maalumu ambao una umeme kwa masaa ishirini na nne, doria haziishi nadani ya gereza hili lenye kila aina ya sifa. Amata alifungwa ndani ya gereza hilo, hakuwahi kufikiri hata siku moja kama angefika mahali pale daima alisikia hadithi tu watu wakisimulia na kusifia sifa mbaya za jingo hilo, aliona kuwa sasa ndio amefika mwisho wa maisha yake, jehanum ya duniani, alikata tama ya kuona tena kijiji chake alichokipenda, watu aliyowapenda, michezo aliyoipenda, shamba lake aliloachiwa na wazazi wake, kila kitu kwake aliona kimefika mwisho na kama kuna kitu alichokichukia tangu muda huo ni Saringo msichana mrembo aliyemhakikishia kufungwa na kuozea jela. ‘Shetani huyu! Shetani mkubwa! Aombe nisitoke ila nifie humu, laiti nikitoka namkatakata vipande na nyama nawapa mbwa wale, naapa’ Amata alijiwazia kwa hasira na uchungu. Akiwa bado ameketi kwenye kigodoro kidogo alisikia sauti ya king’ora hakujua kinahashiria nini alipochungulia katika kadirisha ka mlango aliona wafungwa wote wanakimbilia kwenye uwanja mkubwa, mara mlango wake ukafunguliwa
“haya mfungwa kwenda kwa wenzio haraka!!” sauti ya askari ilimfanya atoke mbio, alifika na kukaa katika mstari paamoja na wengine. Akasimama askari mmoja katikati akiwa na kipaaza sauti “leo ni sherehe!!!!” alitangaza “tunakaribisha wageni na pia tunapunguza wengine” aliongeza, uwanja ulikuwa kimya sana alisikika yeye peke yake
“wale wote waliofika hapa peponi leo waje mstari wa mbele haraka!” alitoa amri
Amata na wenzake saba walisogea mbele wakiwa bado na pingu mikononi, wakasimama mbele, hapo waliweza kuona kila kitu kwa vizuri zaidi.
“kwanza napenda kukukaribisheni hapa Sogera, sehemu takatifu ambayo huna budi kuacha ujinga wako!” aliendelea kusema
 “Mnaowaona hapa wote ni watoto wazuri wenye roho nzuri wasiopenda ujinga!” alisema huku akitafuna big G yake, askari huyu mrefu mpana mwenye tambo la kiaskari hasa aliongea maneno haya bila kuonesha tabasamu wala kutikisika, akiwa na bastola yake kiunoni na sare yake ya magereza iliyomkaa vizuri alionekana si wa kuchezea.
“Nyie was*nge! Mliokuja hapa wiki hii, hii ngome ya mjerumani, ukitaka kuishi vizuri fuata amri kumi za hapa ndani, ukiambiwa inama, inama, usilete ubishi kwani waliopo hapa ni binadamu kama wewe wana mahitaji”alisema askari yule.
 Amata aliposikia maneno hayo alisisimka na mwili ulikufa ganzi, askari yule aliendelea…
“Usije kujaribu kutoroka, zawadi ya kutoroka ni kama hii mtayoiona sasa!!!” akageuka nyuma akapaza sauti “Afande, lete hao!” mara wafungwa wanne waliletwa wakiwa wamefungwa kamba mikononi wakiburuzwa kama magunia, walijaribu kukukuruka lakini haikusaidia. Pale aliposimama askari yule palikua na jukwaa kubwa lenye kitu kama goli la mpira, lakini juu yake kulikuwa na kitu tofauti, ubao mnene mkubwa wenye tundu la nusu duara lakini katika tundu lile kulikuwa na kitu kilichokamilisha duala lile kiling’aa sana kana kwamba kuna chuma katikati, stailess steel, na upande wa chini wa goli hilo kulikuwa na ubao mwingine kama ule lakini huu kwenye tundu lake haukuwa na kile kitu kama chuma. Mfungwa mmoja aliburuzwa mpaka pale na kufungwa kwa kamba katika goli lile akielezewa chini shingo yake ikiwa imepachikwa kwenye ile nusu duara mwili ukiwa upande wa pili na kichwa upande mwingine, mara kibao kile cha juu kilifyatuka na kuteremka kwa kasi, akiwa bado kapigwa na bumbuazi Amata alihisi kitu kama jiwe la duara kikimgonga miguuni na kuhisi maumivu, alipoangalia chini ni kitu gani hakuamini macho yake, kichwa cha mtu kinachovuja damu mbichi kikiwa kimekatwa kutoka kwa mfungwa yule aliyefungwa pale golini, Amata alichanganyikiwa hajawahi maishani mwake kuona kichwa kisicho na kiwiliwili, akaanza kukimbia.
“Kamata huyo!” amri ilitolewa, askari wawili walianza kumkimbiza, alipigwa ngwala lakini kwa umahiri mkubwa Amata aliruka samasoti na kutua kwa miguu miwili kabla hajakaa sawa alistukia kamba iliyorushwa kwa ustadi ikimfunga shingoni, akageuka na kurusha ngumi iliyompata askari yule sawia shavuni, kabla hajakaa sawa alipigwa teke moja la kifua na kuyumba akaangukia katika mtaro wa maji machafu akatoka kwa haraka alipata pigo lingine maridadi lililompoteza kabisa akaanguka tena, askari wale wakamfunga kamba na kumburuza mpaka uwanjani naye akawekwa pamoja na wale wanaosubiri kunyongwa, akafunikwa nguo nyeusi kichwani asiweze kuona chochote.
 “He he he safi sana kijana! Umediriki kufanya kosa ambalo leo litagharimu maisha yako!” askari yule aliyekuwa na kipaza sauti alimwambia amata
“Mleteni mbele!” akasogezwa mbele ya lile jukwaa la kunyongea
“Mtoeni kitambaa!” akatolewa kitambaa
“Mfungueni pingu!” akafunguliwa pingu na kubaki huru. Askari yule akasema “umeonesha ujeuri, umempiga askari wangu, sasa utashughulikiwa ili ujue kuwa hapa ni mahali pa pekee” alimsogelea Amata na kumwangalia usoni
“kwanza umechoka! Mwili na roho! Nani aliyekuleta huku? Leo utajutia ulichowafanyia wananchi huko uraiani!” alisema yule askari huku amemkazia macho Amata, Amata alimwangalia askari huyu mwenye macho mabaya, mekundu na alikuwa kila akiongea mdomoni mwake kulitoka harufu ya tumbaku na gongo. Askari yule alimzunguka Amata kama mara tatu hivi.
“Cockroach! Fanculo! Caputana!” alimtukana Amata kwa lugha ambayo hakuielewa. Amata aliona kuwa sasa mwisho wake umefika.
“Aje mwanaume amshughulikie huyu!” aliita askari yule. Mara akajitokeza pande la mtu, lenye mwili mkubwa, kifua kipana, sura yake ilionesha kila dalili ya kutokuwa na huruma na mtu, lilimsogelea Amata pale alipo, Amata akarudi nyuma kidogo, lile jitu likamsogelea zaidi, Amata alishikwa na hofu ya kifo alipogeuka nyuma akakuta watu tayari wamefanya duara kubwa hamna pa kupenya, alihisi pigo moja la mgongo lililompeleka chini alipojigeuza kuangalia juu aliliona lile jitu likinyanyua mguu kumkanyaga akajiviringisha upande wa pili na jitu lile likakanyaga chini kwa nguvu kishindo ambacho kilitimua vumbi, amata kwa kutumia nguvu zote alirusha teke lililompata nyuma ya magoti jitu lile likajikuta limepiga magoti, Amata alijinyanyua haraka. Kelele za wafungwa za kumshangilia Amata zilimpa nguvu akiwa bado anawaangalia wanaomshangilia alipigwa roba maridadi ambayo ilimkosesha pumzi, Amata alikukuruka aliporusha mguu wake kwa nguvu kwa nyuma alilipiga hilo jitu kwenye maeneo nyeti, jitu likamuachia Amata na kujishika maeneo,Amata akaanguka chini akanyayuka haraka na kwa kasi ya ajabu aliruka kitu kama tik tak akalipiga usoni kwa migu miwili, nguvu ile ilimfanya jitu asimame wima bila kujua lakufanya, Amata kijana aliyejaliwa wepesi na kusaidiwa na michezo ya sarakasi aliyokuwa akicheza shuleni aliruka hewani na kumpiga mateke ya kifua, jitu lile lilidaka miguu ya Amata kwa ustadi lakini Amata alijikunja kama samaki na kumpiga kichwa usawa wa pua na kumvunja mfupa wa pua, Amata alianguka chini baada ya kuachiwa na lile jitu ambalo wakati huo lilikuwa linavuja damu puani likiwa limeshika pua, Amata alisogea na kurusha makonde mfululizo yaliyokwenda sawia tumboni ambapo jitu lile liliachia uso na kujishika tumboni na Amata alibadili mashambulizi kupeleka usoni, alitumia mtindo huo kama dakika mbili mpaka jitu lile likawa hoi kabisa. Kelele za wafungwa zikazidi kuufunika uwanja wote askari wakaja kumkamata Amata na kumtoa asije akaleta madhara zaidi.
Masikini Amata, hakujua kuwa aliyempiga ndiye mbabe wa gereza hilo, hakuna na haijawahi kutokea mtu akamshinda, wafungwa walimshangilia Amata na tangu hapo akawa na marafiki wengi na kuogopwa na wafungwa wengine.

**************
Maisha yaliendelea gerezani miezi sita ikapita, kazi, mateso, uonevu ndio ilikuwa sera ya maisha yao na Amata akazoea hali hii, kila kukicha hawaishi kupigana na kuumizana kunyang’anyana vyakula na kutaka kuwageuza wenzao, japo Amata hakupenda hali hiyo.

Ilikuwa asubuhi tulivu sana jumapili fulani, watu wengi walikuja kuwatembelea ndugu zao. Amata alikaa kwenye gogo lililopo ndani ya gereza hilo akitafakari hili na lile akimkumbuka huyu na yule. Mara alihisi gogo lile kutikisika alipogeuka alimuona mfungwa mwingine amekaa jirani naye, Amata  akamtazama jamaa yule kwa makini sura yake haikuwa ngeni sana lakini hakukumbuka amemuona wapi, alimtazama tena na tena.
“Rafiki!” mfungwa yule alimuita Amata kwa sauti ya chini, Amata akaigeuka tena kumwangalia vizuri usoni, Amata akaingiwa na hofu kidogo maana mfungwa huyu hajawahi kukutana naye sura yake ya kawaida tu lakini alipotabasamu aligundua kuwa hakuwa na meno, Amata alisogea pembeni kidogo akamuuliza
 “wewe ni nani, mbona sijawahi kukuona?”
“Umenisahau?! Wewe ni Amata Ga Imba siyo?” Amata alishtuka kuona hata jina lake analijua.
“Ndiyo! Mimi ni Amata Ga Imba mwana wa Nkhunulaindo! Nikusaidie nini?” Amata alijibu na kuuliza kishari kwa maana ndiyo hali aliyoizoea sasa.
“Mimi naitwa Golam wa Golam!” alijitambulisha kwa Amata, kasha akatoa lile tabasamu lake ambalo lilimfurahisha Amata hata alitamani kucheka, kwa sababu kweli alifanana na Golam ambaye amata aliwahi kumuona katika filam huko kijijini kwao.
“Safari imewadia!” Golam alimnong’oneza Amata
“Safari, safari gani?” Aliuliza kwa mshangao lakini kwa sauti ya chini
“Mimi na wewe tuna safari ya mbali na ngumu sana, safari hii itatugharimu mengi sana lakini mwisho wake tutaishi kama wafalme he he he! Nilikuwa nakungoja, na sasa umefika. Wewe ni Mate ya Simba, kila mnyama atakukimbia, mapori yote yatakuinamia na kukuheshimu, funga mkanda Amata, safari imewadia” Golam aliongea kwa utulivu mkubwa. Amata hakuelewa anachoambiwa wala anachokisikia, aliduwaa tu akitazama upande wapili jinsi pilikapilika za wafungwa na askari zilivyoendelea
“Unat…” alitaka kumuuliza Golam lakini alipogeuka hakumuona, Golam alishaondoka pale kitambo na Amata hakuweza kujua ameenda wapi! Amata aliona kama katokewa na shetani la kiume, ‘safari, safari gani, kwenda wapi? Lini? Mh!’ hakuweza kupata jibu juu ya maswali hayo, alinyanyuka pale alipoketi na kuvuta hatua chache kuelekea lango kuu la gereza, alichokiona hakukiamini, ‘Saringo!’ alishaangaa, mara aliitwa kuonana na mgeni wake, alikataa kwenda akamwambia afande kuwa hana mgeni, afande akamsisitizia kwa kuwa alishapewa pesa kidogo na Saringo ili afanye makeke, kwa kuwa wafungwa wa aina ya Amata hawakutakiwa kuonana na ndugu ovyo. Alikwenda lakini moyoni mwake hakutaka maishani kuonana na kiumbe huyu mwenye uzuri uliofunika unyama wake.
“Unataka nini tena? Nimeshafungwa! Unataka kuniambia kuwa nitanyongwa, sivyo?” amata alimwambia Saringo.
“Amata! Nimekuja kukuomba msamaha, maneno yale sikutegemea kama yatakuwa kweli, wewe hunijui wala mimi sikujui ila nilitumwa kwako na aliyenituma anakuhitaji sasa!” saringo aliongea kwa uchungu akimwangalia Amata machoni mwake. Kisha akaingiza mkono kwenye pochi yake akatoa kikaratasi cha rangi ya purple kimekunjwakunjwa akatazama huku na huku akamkabidhi Amata, Amata akakipokea akakificha kwenye nguo ya ndani. Saringo akatoa tabasamu la nguvu kwa Amata, kisha akageuka na kuondoka zake, Amata alibaki anamwangalia akifarijika kuona jinsi mtoto huyu alivyojaaliwa hata upande wa nyuma ‘mashaallah’ alijisemea moyoni, mara alijikuta vurugu kubwa inatokea ndani ya suruali yake ya orange akagundua kuwa macho yamemponza, akarudi ndani.
Jumapili hiyo ilikuwa ni siku ya burudani na michezo huwa mara moja kwa miezi mitatu, Amata akaketi kwenye nyasi akiangalia wafungwa wenzake wakisakata kabumbu, kila alipoangalia huku na huku hakumuona Golam, alishindwa kujua kama Golam alikuwa mzuka au mfungwa mwenzake, mara akaanza kucheka mwenyewe alipokumbuka tabasamu la Golam. Aliondoka eneo hilo na kusogea pembeni huku akimuangalia kila anayekutana naye labda atamuona lakini hakufanikiwa, aliendelea kuvuta hatua taratibu akiwa bado na mawazo lukuki na maswali yasiyo na majibu.

Golam wa Golam, mfungwa asiyependa kuongea sana na anayependa kufanya kazi muda wote, alikuwa amepangwa kufanya kazi jikoni kama mpishi na kwa miaka miwili sasa. Golam alifungwa katika gereza la Sogera yapata miaka saba sasa kwa kosa la mauaji, alikuwa hapo akisubiri hukumu yake ya kunyongwa kwa kosa hilo. Alipokuwa gerezani humo hakupenda kujichanganya na wafungwa wengine hakuwa na rafiki na daima alionekana mtu mwenye kupanga kitu fulani, kwa kipindi cha miaka saba hii hata ndugu zake walishajua kuwa amenyongwa, hawakuja kumtazama wala kumtaka hali. Alipata kufahamu njia zote za gereza hilo na ratiba zote za askari za ulinzi wa gereza hilo. Aliwahi kuwa na rafiki mmoja tu ambaye yeye alishanyongwa pale tu alipojaribu kutoroka kwenye ngome hii isiyopenyeka.
Akiwa bize na kazi ya kuandaa chakula cha jioni cha siku hiyo Golam alionekana mtulivu sana hata alikuwa anafanya kazi dakika chache na chache anapumzika lakini akizama katika fikra zingine.

Amata alirudi kwenye kichumba chake na kujilaza kwenye kigodoro chake kidogo, baridi ilikuwa kali sana siku hiyo, akiwa amejilaza hapo alipitiwa na usingizi.
‘Watu warefu walikuja wakamkamata Amata, wakambeba juu juu, watu hao Amata hakuweza kuwaona miguu yao wala sura zao, walimpitisha kwenye bonde kubwa lenye manyoka makubwa mengine yana vichwa viwili, manyoka yale yalijaribu kumrukia lakini kutokana na urefu wa hao viumbe waliombeba hawakuweza kumfikia kabisa. Mara walifika eneo kubwa la wazi, pale aliona viumbe wenye vichwa vibaya na vipembe vilivyojinyonga kama vya kondoo, katikati yao kulikuwa na chungu kikubwa kinachotoa mvuke wa ajabu. Mara wale viumbe waliombeba walianza kuwa wafupi mpaka kufikia urefu wa wale wengine, walimpomshusha, Amata ndio aligundua kuwa wale viumbe wana miguu kama ya kuku na mikia pia walikuwa na jicho moja, wakamnyanyua ili kumtumbukiza ndani ya chungu, kumbe hawa viumbe wanakula watu baada tu ya kuwachemsha, Amata alipiga kelele za ajabu….’
Mara alikurupuka kutoka usingizini kumbe alipitiwa na ndoto ya ajabu na mbaya. Jasho lilimvuja kama kamwagikiwa na maji, akitweta kama mtu aliyekimbia mbio fupi za mita mia moja. Alipotulia na kurudi katika hali ya kawaida huku akijiuliza maana ya ndoto hiyo aliona kipande cha karatasi chakavu chini ya mlango, alijinyanyua taratibu na kuokota kikaratasi kile, akakifungua kwa woga, kikaratasi kile kilikuwa kichafu lakini kwa taabu aliweza ona kilichoandikwa kwa muandiko ambao herufi zake ziko mbalimbali, alijaribu kuziangalia vizuri lakini ilimuia ngumu kuelewa ni nini kimeandikwa, alikiweka pembeni, alipoangalia nje kupitia kidirisha kidogo aliona bado ni usiku kwani ni mbala mwezi na nyota ndizo zilizong’aza nje, na mizunguko ya askari walio zamu kwa muda huo. Aliketi tena juu ya kigodolo chake akakunjua tena kijikaratasi kile, alipokigeuza kwa nyuma aliona mchoro wa ajabu, hakuweza kuuelewa mchoro huo, kitu chenye umbo la mraba, ndani yake kuna duara kubwa ambalo lililochorwa X, katikati ya x ile pamewekwa namba tano na mshale uliongalia juu, kabla ya kuishia mshale ule kamstari kengine kalikatisha na kufanya kitu kama mchoro wa dira katika kamstari kale kuliwekwa herufi A upande wa kulia na kuliandikwa lugha isiyoeleweka, Amata aliangalia mchoro ule akaona hamna anachokielewa akakunja kile kikaratasi tena akakiweka chini ya tandiko akajilaza.
Kulipopambazuka siku hiyo Amata aligubikwa na mawazo mengi alikuwa mpole sana kama mtu anayeumwa, siku hiyo alitakiwa kwenda na wafungwa wenzake kukata miti kwa ajili ya kuongeza idadi ya kuni kwa matumizi ya gereza. Wakiwa msituni na kazi imepamba moto, waliendelea na kuimba nyimbo mbalimbali za kuhamasishana huku wengine wakipakia magogo lorini, askari mmoja bwana mdogo alisogea karibu na Amata
“Mfungwa! Chagua wengine watatu tukashushe mzigo wengine endelea…”alimwambia Amata. Wafungwa wanne wakapanda pamoja na Amata, akiwa amekaa juu kabisa ya lori lile pamoja na askari wawili wenye SMG wakiwa makini na kazi yao, lori lile aina ya Leyland lilikwenda kwa mwendo wa pole likiwa linapanda mlima mkubwa sana. Lilipofika juu yam lima kabla alijaanza kuteremkia upande wa pili, Amata aligutushwa na mfungwa mwingine
“Amata! Cheki nyuma ile yako bondeni ilivo…” alimwambia. Amata akaangalia kwa makini akaweza kuliona gereza ambalo wenyewe huliita nyumba, akaangalia vizuri, lilikuwa linaonekana bondeni hivyo aliweza kuliona vizuri sana. Mara akaona kitu cha ajabu kidogo aliweza kuiona vizuri picha ya gereza lile… aliliona katika mraba na alipokaza macho aliona kwa ndani kuna kama kitu cha duara kilichozunguka, Amata alishangaa sana akaingiza mkono kwenye nguo yake ya ndani akatoa kile kikaratasi mara akakumbuka kuwa alipo hapafai kufanya hivyo
“Mfungwa! Telemka huko kaa chini na wenzio!” aling’aka kwa hasira akimnyooshea kiboko chake. Amata alishuka na kujichanganya na wengine.
Safari ilitimu wakashuka na kuanza kutelemsha kuni kupeleka jikoni, alipoingia jikoni alimuona Golam kwa mbali akiwa ametingwa na kazi. Golam nae akamuona Amata, akatoa lile tabasamu lake, Amata akamsogelea Golam
“Umeona mzigo wako?” Golan alimuuliza Amata kwa sauti ya chini huku wakipanga kuni
“Mzigo gani?”Amata akauliza
“Karatasi ndogo” Golam akajibu
“Ndio! Ni nini kile? Sijaelewa” Amata alimuuliza
“Mimi sijui! Nimepewa nikuletee” alijibu Golam
“Oooh nani alikupa?” Akauliza Amata
“Amesema utamkuta, muonane” Golam alimueleza
“Nitamkuta wapi? Nani?” Amata alizidi kuchanganyikiwa kabla hajauliza aliitwa na askari na wakaondoka. 

Mvua kubwa ilinyesha jioni ile radi kali zenye ngurumo za ajabu zilendelea. Amata na wenzake walikuwa bado wapo kazini, sasa walikuwa wakirekebisha mitaro ya maji machafu , viatu walivyovaa vilikuwa vimelowa alkadhalika nguo zao zilikuwa chapachapa huku baridi kali ikiwapiga walifanya kazi chini ya uangalizi mkali tena wakati kama huu walifungwa minyororo miguuni. Baada ya kazi hiyo ilipigwa filimbi na wote walitakiwa kusimama katikati ya uwanja ule. Amata akiwa katikati kabisa ambapo nyuma yao kidogo kulikuwa ni sehemu ya kunyongea, mara akasikia sauti ya kitu kama jiwe liliodondokea batini upande wa kushoto akageuka upande ule, kulikuwa na kibanda kidogo kilichotumika kama choo kwa ajili ya askari, akufuatilia sana akageuka kuangalia mbele lakini kuna kitu kilimrudisha macho upande ule, katika mlango wa choo kile kulikuwa na mchoro wa pembetatu iliyojazwa rangi na katikati kulikuwa na duara ambalo halikupakwa rangi, mchoro ule ulimvutia Amata akakumbuka katika kile kijikaratasi upande wa nyuma kuna ule mchoro hapo akagundua lazima kuna siri ndani yake kwa nini michoro hii ifanane, hapo akavuta taswira akakumbuka jinsi alivyoona gereza lile kwa juu wakiwa juu ya mlima akaoanisha hivi vitu vitatu akagundua kuna siri ndani yake ‘labda Golam anafahamu siri hii’ alifikiria moyoni. Mvua kubwa iliendelea kunyesha
“Kutokana na hali ilivyo hatuwezi kuendelea na kazi” aliwaambia askari mmoja, kasha akaendelea
“mtapanga foleni mtachukua chakula na kwenda kupumzika, hatakiwi mtu kuonekana nje!”
Wakiwa katika foleni ya chakula, Amata alikazia macho sana upande ule, alikuwa bado anatafiti kichwani mwake ni kwa nini michoro ile ilifanana na ile ya kwenye kijikaratsi kile kinachoonekana kuchakaa sana pia ni kipande tu je kingine chake kikowapi, alikosa jibu.

**************

Usiku ule tafrija ya maafande iliendelea, pombe za kufa mtu zilikuwa huko, Amata alikuwa ni mmoja wanaosaidia katika tafrija hiyo, lakini akili yake yote ilikuwa ni kuingia ndani ya choo kile aone tu kuna nini, kwa mbali alimuona Golam nae yuko bize kuhudumia katika meza ya wakubwa, brassband iliendelea kupiga mziki wa taratibu. Amata alijaribu kuangalia ulinzi uliopo muda huo aliona hakuna mabadiliko kabisa lakini alijaribu kutafuta nafasi japo aonane na Golam.
Alipokuwa stoo akipanga vinywaji kwenye chano mara Golam aliingia moja kwa moja akamfuata Amata
“Tutafute muda tukajisaidie!” alimnong’oneza Amata. Amata akapokea kwa mshangao kauli hiyo lakini baadae akaona kuwa lazima Golam anafahamu chochote juu ya choo kile.
“Wakianza kuchangamka tu tuonane ili tujue tunaingiaje pale chooni, maana kwa nyuma kuna mlinzi na juu kabisa yupo mwingi na taa kubwa inamulika ule mlango” Golam aliendelea kumdokezea Amata. Akili ya amata ilianza kufanya kazi kwa kasi na shauku ya kuingia pale ilimjaa, lakini aliwaza ‘vipi wasipokuta chochote mle ndani na wakasthukiwa na askari, itakuwaje’ alikumbuka yule jamaa jinsi alivyonyongwa akaingiwa na woga. Lakini alijipa moyo na kuamua kutoa dozi ya pombe ili hawa jamaa wachangamke mapema.
Punde si punde, sherehe ilichangamka, watu waliimba na kucheza, Golam akazunguka upande wa Amata akampigia mbinja, Amata alipogeuka akamuona Golam, Golam akampa ishara ya mkono kuwa azunguke upande wa pili wa jingo hilo, alipofika upande huo alikuta miili miwili ya askari ikiwa chini, Golam akamwambia Amata avae uniform ya mmoja wao, akafanya hivyo japo nguo ile haikumkaa sawia lakini alionekana kama mmoja wa maafande, Golam naye akatwaa za yule mwingine halafu wakawavalisha nguo zile za ufungwa, amata hakujivunga akabeba SMG na magazine mbili za akiba akamuoneshea alama ya dole gumba
“Naingia vitani!” Amata alinong’ona kwa Golam. Golam aliondokea upande wa pili na Amata upande mwingine, kazi ikaanza.
Hadi kufika katika choo kile kutoka walipo akina Amata ni kama mita mia nne hivi na katikati hapo kuna mataa makubwa yanayoangaza hata akipita panya taa zile huzungushwa kufuatilia kinapoelekea kitu hiko, jinsi walinzi walivyo makini. Amata akajiweka tayari na kwa mwendo wa taratibu akiwa amejifunika koti lile la magereza, alivyojipapasa mfukoni alikuta kuna sigara alipoitoa aligundua kuwa ni msokoto wa bangi, Amata akatabasamu kwa sababu ana muda mrefu sana bila kupata hiyo kitu. Aliendelea kupita na kiambaza cha ukuta chini ya vibanda vya walinzi, alipofika upande ule ambako ndiko choo kile kilipo alitulia kidogo kwenye kona moja kwa kuwa aliona mtu akija upande ule aliokuwepo. Amata alisimama kikakamavu akiwa kampa mgongo mara alihisi kashikwa begani alipogeuka taratibu aligundua alimgundua kuwa alikuwa Golam
“Shhhhhh!!!” Golam alimuashiria Amata kutulia kisha akampita na kumpa ishara ya kumfuata, Amata alimfuata kwa nyuma wakazunguka nyuma ya jengo ambalo hutumika kama stoo ya kuni wakalipita na kuendelea mbele kisha Golam akasimama juu ya kitu kama tank kubwa liliochimbiwa ardhini, akatoa katochi kadogo kama peni ambako alikakuta ndani yan nguo zile akamulika juu ya mfuniko wa taki lile, kulikuwa na matenki kama matano. Amata hakuelewa Golam anaangalia nini juu ya matank hayo, tank la tatu akamwita Amata kasha akampa ishara ya mkono kumuonesha kwamba ‘ni hapa’, Amata na Golam wakasaidiana kufungua mfuniko hule na walipofanikiwa Golam aliingia wa kwanza na Amata akafuatia kasha wakafunga mfuniko ule kwa ndani.  

Ndani ya shimo lile kulikuwa na giza nene sana hata huwezi kuona kitu kilicho mita moja mbele yako, Amata alijaribu kukanyaga taratibu na Golam akafuatia, Golam akatoa katochi kake mfukoni na kuangaza kidogo, ni mwanga hafifu sana uliotoka katika tochi ile haikuweza kuangaza mbali, taratibu Amata alimfuata Golam alikoelekea kwa mwendo wa kunyata, ukimya uliokuwa ndani ya shimo lile ulitisha, kawa mwendo ule ule wakiangaziwa na mwanga hafifu, Amata aliogopa sana kutokana na giza lile alitamani kumwambia kitu Golam lakini alishindwa pia aliona labda akifanya hivyo ataaribu utaratibu asioujua, mara ghafla wakasikia kelele kama za mbawa za njiwa arukae kabla Amata hajajiweka tayari Popo mkubwa alipita usoni kwake na mbawa zake zikampiga usoni, Amata alitoa mguno wa sikitiko lakini hakuthubutu kupiga kelele alivumilia tu, bado waliendelea kupiga hatua ndogondogo. Baada ya kutembea kwa mwendo huo kama dakika kumi na tano hivi Golam akasimama ghafla kisha akamzuia Amata kwa mkono wake walisimama katika ukimya wa hali ya juu kama sekunde hamsini hivi. Amata alitamani kumuuliza kitu Golam lakini bado alishindwa ila alihisi kitu fulani kumkaba kooni kutaka kusema lakini aliona sio wakati muafaka japo alipenda kujua hata ni wapi wanaelekea.Walitembea taratibu mwendo kama wa lisaa limoja, masikio ya Amata yalikuwa kama yanataka kuziba kwa ukimya ule ambao hajawahi kuuhisi katika maisha yake, mara akaanza kusikia sauti kama za njiwa dume na jike wakiwa katika harakati za mapenzi na punde tu zikapotea akaanza kusikia sauti za mbu wengi sana wakitaka kuingia masikioni lakini alipopunga mkono wake upande wa sikio hakuhisi kugusa chochote akasikia kama wanamfuata kwa nyuma akageuka hakuona kitu huku akivuta hatua ndogondogo mara akahisi kugonga kitu alipotazama mbele alijikuta amegonga ukuta... hakuna njia... Golam haonekani! Matatizo.
Amata alipapasa ukuta ule akona ulikuwa wa mawe makubwa ambayo si ya kujengwa na binadamu bali ni mwamba mkubwa, mkono wa mtu ukamshika begani Amata akashtuka na kupiga ukelele wa nguvu alipogeuka alimuona Golam,
“Usipige kelele !!” Golam akamsisitiza Amata
“Utawaamsha mapema!” aliongeza
Amata hakuelewa alichoambiwa na Golam ‘nani wataamka mapema?’ alijiuliza bila jibu
Mbele kidogo walikuta kuna milango milango ipatayo kama nane hivi, Golam akasimama akatoa kipande cha karatasi kutoka kwenye nguo yake ya ndani akakimulika kwa mwanga hafifu wa kale katochi ambako tayari betri zake zilishaanza kupoteza nguvu. Golam akawa kama anahesabu kitu fulani katika ile milango kisha akampa ishara ya kumfuata Amata akafanya hivyo, walipita kwenye moja ya hiyo milango huko wakatembea kwa mwendo wa haraka kidogo, Amata aliendelea kusikia sauti za vitu mbalimbali mara watu wanacheka mara wanalia, kwake ilikuwa ni uoga mtupu. Mbele kidogo baada ya mwendo wa kama saa moja ingine Amata alianza kusikia kelele za maji mengi kama mto upitao, akamtazama Golam ambaye alikuwa amesimama kimya kama gogo, akamsogelea akamuona Golam kafumba macho katulia sana hakumshtua akasubiri aone nini kinafuata.
“Maji !” Golam alinong’ona na Amata akasikia mnong’ono huo
“Sasa tufanyeje?...”Amata naye alijibu kwa swali kwa kunong’ona
“Lazima tuvuke, tufuate huu mto... mto Solondo” Golam alimjibu Amata
“Mto Solando!?” Amata alishangaa na kumuuliza Golam
“Ndiyo. Huu ni mto wa Solondo, lazima tuvuke kwa kuogelea kuna watu wanatusubiri nje, ila tahadhali mto huu una Mamba na maajabu mengi uwe makini, unajua kuogelea?” Golam akamwambia Amata
“Najua kidogo sijawahi kuogelea kwenye maji mengi kama haya, hakika nitakufa.” Amata alijibu kwa kuhuzunika
“Acha ujinga Amata! Ukisema utakufa, utakufa kweli” Golam alimwambia Amata kwa ukali kidogo na kumtupia swali
“haya unajua haya maji yanaelekea upande gani?”
Amata kwa uoga akajibu
“Sijui mbona hata maji yenyewe siyaoni nasikia mvumo tu”
“Ukipiga hatua mbili utatumbukia mtoni. Niambie haya maji yanaelekea upande gani? Tunatakiwa kuelekea upande yanakotoka siyo yanakokwenda...” Golam aliendelea kumuambia Amata.
Golam akachuchumaa na Amata akafanya vivyo hivyo,
“Papasa kwa mkono polepole mpaka ufike ukingo wa mto kisha tumbukiza japo kidole uone maji yanaelekea wapi!” Golam alimwambia Amata. Amata akafany hivyo akapapasa na mara akahisi kafika mwisho wa kajia kale na kelele za maji ziliongezeka, akaingiwa na woga mkuu, moyo wake ulikuwa unadunda kwa kasi na kijasho kumtiririka. Akayagusa yale maji yalikuwa ya moto kama yako jikoni akahisi mkono wake unavutwa upande wa kulia, akajaribu kuutoa alihisi kama kitu kimemshika mkono kinamvuta majini, nguvu zikamuishia akapiga kelele
“Golaaaaaaaammmmmmmmm!!!”
Kishindo kikubwa kikasikika cha kitu kutumbukia majini, Golam akapiga hatua mbili mbele akaita
“Amataaaaaa!!!”
Alipoona kimya akajirusha majini akapiga mbizi maridadi, ndani yamaji yake palikuwa na mimea iliyotambaa akamuona Amata amenasa kwenye mimea hiyo akaogelea na kuanza kumsaidia aktoa kisu chake kidogo na kuanza kukata mimea hile, kila alipokata ilitoa kitu kama damu, alipofanikiwa kumto Amata wakaanza kuogelea kinyume na maji haikuwa kazi ndogo. Amata hakuwa mzuri kuogelea kama Golam kila mara Golam alijikuta kamuacha Amata nyuma, Golama akamshika Amata huku upande mmoja kashika kwenye ncha ya jiwe akamvuta Amata kwa nguvu zote na kumuweka mbele yake, wakaendelea kuogelea sasa Amata akiwa mbele na Golam nyuma. Amata akiwa mbele aliendele a kuogelea kwa shida kwa kuwa maji yalikuwa yanasukuma nyuma, Golam alijitahidi kumlinda Amata asije kubebwa na maji. Baada ya kuogelea kama masaa mawili hivi Amata alianza kuona maji yale yanang’aa kwa mwanga wa nje, alikuwa amechoka hata kujisogeza haikuwa rahisi, Golama alimvuta Amata na taratibu walijikuta wanafika nje ya lile pango kubwa lakini bado kasi ya maji haikuwa ndogo, Amata akahisi kitu kimemshika mguu akahangaika kujinasua akashindwa, Golam akajitahidi kumvuta lakini haikuwa rahisi wote walikuwa wamechoka sana, Amata akaponyoka kutoka katika mikono ya Golam, akahisi kuvutwa tena majini mara hii ni kwa nguvu zaidi, alihisi kama mikono ya watu imemshika miguu, alikunya maji akajaribu kujizuia lakini ikashindikana alilegea na kukosa nguvu kabisa. Golam aliibuka nje ya mto, akarushiwa kamba na kuishika barabara akavutiwa nje
“Amata yuko wapi?” aliulizwa, akajibu kwa ishara tu kuoneshea kuwa yuko ndani ya maji. Jiwe kubwa lililosukumwa na maji lilimgonga Amata kwenye paji la uso akachanika ngozi ya usoni damu zikaanza kumvuja kwa nguvu, mara akajikuta ameibuka nje na kunaswa kwenye miti midogo iliyo jirani na hapo, Golam akamuona Amata, wakafanya juu chini na kumnasua na kumleta nchi kavu. Wakakoka moto mkubwa ili kuwapa joto Golam na Amata, wakamsaidia Amata kutapika maji yale na kuzuia damu iliyokuwa inatoka katika jeraha lake. Amata akapoteza fahamu.

                                                       *******************

 je ni akina nani waliowasaidia kuwatoa katika maji?
Safari hii ni ya kwenda wapi?

Usikose sehemu ya pili ya simulizi hii ya kusisimua... jiunge na msimulizi wako Amata Ga Imba...